Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nane · Mabunge

Kifungu cha 124

Kif.124

Kamati na Sheria Zinazosimamia Vikao vya Bunge

(1)Kila Kitengo cha Bunge kinaweza kubuni kamati, na kitaweka Kanuni za Vikao vya Bunge ili kuendesha vikao kwa utaratibu, ikijumuisha vikao vya kamati za kitengo hicho.

(2)Bunge linaweza kubuni kamati za pamoja zinazojumuisha wanachama wa Vitengo vyote viwili vya Bunge na inaweza kudhibiti kwa pamoja utaratibu wa kamati hizo.

(3)Vikao vya Kitengo chochote cha Bunge havifanywi kuwa haramu kwa sababu tu ya—

(a)nafasi katika uanachama wake; au

(b)kuwepo au kushiriki kwa mtu yeyote asiyepaswa kuwepo au kushiriki katika vikao hivyo vya Kitengo hicho.

(4)Kitengo cha Bunge kinapozingatia uteuzi wowote ambao kuidhinishwa kwake kunahitajika chini ya Katiba hii au Sheria ya Bunge––

(a)uteuzi huo utashughulikiwa na kamati husika ya Bunge;

(b)mapendekezo ya kamati yatawasilishwa katika Kitengo hicho cha Bunge ili kuidhinishwa; na

(c)vikao vya kamati na vya Bunge vitakuwa wazi kwa umma.

Isome ndani ya Sura ya Nane →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho