Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nane · Mabunge

Kifungu cha 127

Kif.127

Tume ya Huduma za Bunge

(1)Tume ya Huduma za Bunge Imebuniwa.

(2)Tume hiyo inajumuisha—

(a)Spika wa Bunge la Kitaifa, kama mwenyekiti;

(b)naibu mwenyekiti aliyechaguliwa na Tume kutoka kwa wanachama walioteuliwa kwa mujibu wa kifungu cha (c);

(c)wanachama saba walioteuliwa na Bunge kutoka miongoni mwa wabunge na ambao—

(i)wanne watateuliwa kwa usawa na chama au muungano wa vyama vinavyounda serikali ya kitaifa vilivyo katika Bunge na ambao angalau wawili kati yao watakuwa wanawake; na

(ii)watatu watateuliwa na vyama visivyo kwenye serikali ya kitaifa, angalau mmoja akiteuliwa kutoka kila Kitengo cha Bunge, na angalau mmoja wao akiwa mwanamke; na

(d)Mwanaume mmoja na mwanamke mmoja aliyeteuliwa na Bunge kutoka miongoni mwa watu ambao sio wabunge lakini wana uzoefu mkubwa katika masuala ya umma.

(3)Karani wa Seneti atakuwa Katibu wa Tume hiyo.

(4)Mwanachama wa Tume ataondoka ofisini—

(a)ikiwa mtu huyo ni Mbunge—

(i)baada ya kukamilika kwa muhula wa Kitengo cha Bunge ambacho mtu huyo alikuwa mbunge;

(ii)ikiwa mtu huyo atawacha kuwa Mbunge; au

(b)ikiwa mtu huyo ni mbunge mteule, baada ya kuondolewa kwa uteuzi wake na Bunge.

(5)Licha ya Ibara ya (4), muhula wa Kitengo cha Bunge unapokwisha, mwanachama wa Tume aliyeteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2) (c) ataendelea kuhudumu ofisini hadi mwanachama mwingine atakapoteuliwa na Bunge litakalofuata ili kuchukua nafasi yake.

(6)Tume ina jukumu la—

(a)kutoa huduma na msaada ili kufanikisha utendakazi bora na wenye ufanisi wa Bunge;

(b)kubuni ofisi katika huduma ya Bunge, na kuteua na kuwasimamia wanaohudumu katika ofisi hizo;

(c)kutayarisha makadirio ya matumizi ya fedha ya kila mwaka katika huduma za Bunge la Kitaifa na kuyawasilisha kwa Bunge la Kitaifa, na kudhibiti bajeti kuhusu huduma hizo;

(d)Kuanzisha kibinafsi au kwa pamoja na mashirika husika, mipango ya kukuza maadili ya demokrasia ya bunge; na

(e)kutekeleza majukumu mengine—

(i)ambayo ni muhimu kwa manufaa ya wabunge na wafanyakazi wa Bunge; au

(ii)yatakayotolewa na sheria ya kitaifa.

Isome ndani ya Sura ya Nane →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho