Kuondolewa kwa Rais kwa misingi ya kukosa uwezo
(1)Mwanachama wa Bunge la Kitaifa anaweza kuwasilisha hoja Bungeni, ya kuchunguzwa kwa uwezo wa afya ya kiakili au ya kimwili ya Rais katika kutekeleza majukumu ya ofisi yake ikiwa ataungwa mkono na robo ya idadi ya wabunge wote.
(2)Ikiwa hoja chini ya ibara ya (1) itaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa—
(a)Spika wa Bunge atamjulisha Jaji Mkuu kuhusu uamuzi huo katika kipindi cha siku mbili; na
(b)Rais ataendelea kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo kabla ya matokeo ya taratibu zinazohitajika katika Kifungu hiki.
(3)Katika muda wa siku saba baada ya kupokea notisi ya uamuzi huo kutoka kwa Spika, Jaji Mkuu atateua kikundi cha watu watakaosikiza na kuamua swala hilo, ikijumuisha—
(a)watu watatu ambao wanastahiki kuhudumu kama matabibu chini ya sheria za Kenya, na walioteuliwa na taasisi ambayo kwa kisheria inawajibika katika kudhibiti taaluma ya utabibu;
(b)wakili mmoja wa Mahakama Kuu aliyeteuliwa na taasisi ambayo kisheria inawajibika katika kudhibiti utendakazi katika taaluma ya mawakili; na
(c)mtu mmoja atakayeteuliwa na Rais.
(4)Ikiwa Jaji Mkuu atashindwa kuteua kikundi hiki chini ya ibara ya (3) , Naibu Jaji Mkuu atakiteua kikundi hicho.
(5)Ikiwa Rais atashindwa kumteua mtu anayehitajika kuteuliwa chini ya ibara ya (3) (c), mtu huyo atateuliwa na––
(a)mwanafamilia katika familia ya Rais; au
(b)ikiwa hakuna mwanafamilia yeyote ambaye yuko tayari au ana uwezo wa kufanya uteuzi huo, uteuzi huo utafanya na jamaa wa karibu wa Rais.
(6)Kikundi hicho kitachunguza suala hilo na kuripoti kwa Jaji Mkuu na Spika wa Bunge la Kitaifa katika muda wa siku kumi na nne baada ya kuteuliwa.
(7)Spika atawasilisha ripoti hiyo ya kikundi kilichoteuliwa mbele ya Bunge la Kitaifa katika kipindi cha muda wa siku saba baada ya kuipokea.
(8)Ripoti hiyo ya kikundi kilichoteuliwa itakuwa ya mwisho na isiyoweza kukatiwa rufaa na ikiwa kikundi hicho kitaripoti kwamba Rais ana uwezo wa kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo, Spika wa Bunge la Kitaifa atatangaza ripoti hiyo katika Bunge la Kitaifa.
(9)Ikiwa kikundi hicho kitaripoti kwamba Rais hana uwezo wa kutekeleleza majukumu ya ofisi hiyo, Bunge la Kitaifa litapiga kura ya kuidhinisha au kutoidhinisha ripoti hiyo.
(10)Ikiwa idadi kubwa ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa watapiga kura ya kuunga mkono kuidhinishwa kwa ripoti hiyo, Rais atang’atuka mamlakani.