Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi · Kitengo cha Serikali Kinachosimamia Mahakama

Kifungu cha 163

Kif.163

Mahakama ya Juu Zaidi

(1)Mahakama ya Juu Zaidi imebuniwa, na itajumuisha—

(a)Jaji Mkuu, ambaye atakuwa rais wa mahakama hiyo;

(b)Naibu Jaji Mkuu, ambaye—

(i)atakuwa naibu wa Jaji Mkuu; na

(ii)atakuwa naibu wa rais wa mahakama hiyo; na

(c)majaji wengine watano.

(2)Katika usikilizaji wa kesi, mahakama itakuwa imepangwa vizuri ikiwa itakuwa na majaji watano.

(3)Mahakama ya Juu Zaidi—

(a)itakuwa na mamlaka ya kipekee na ya kiasili ya kusikiliza na kuamua kesi zinazohusu uchaguzi wa urais chini ya Kifungu cha 140; na

(b)Kwa kuzingatia ibara ya (4) na (5), itakuwa na mamlaka ya rufaa ya kusikiliza na kuamua rufaa kutoka—

(i)Mahakama ya Rufaa; na

(ii)mahakama nyingine yoyote au taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama itakavyoagizwa kupitia kwa sheria ya kitaifa.

(4)Kukatwa Rufaa kutatoka Mahakama ya Rufaa hadi Mahakama ya Juu Zaidi—

(a)kwa msingi wa haki katika kesi yoyote inayohusiana na ufasiri na utekelezaji wa Katiba hii; na

(b)katika kesi nyingine yoyote ambayo Mahakama ya Juu Zaidi au Mahakama ya Rufaa itathibitisha kwamba suala lililohusishwa lina umuhimu wa kijumla kwa umma, lakini kwa kuzingatia ibara ya (5).

(5)Uthibitisho wa Mahakama ya Rufaa chini ya ibara ya (4) (b) unaweza kukaguliwa na Mahakama ya Juu Zaidi, na kisha kukubaliwa, kurekebishwa au kufutiliwa mbali.

(6)Mahakama ya Juu Zaidi inaweza kutoa maoni ya ushauri kwa serikali ya kitaifa, kitengo chochote cha Serikali, au kwa serikali yoyote ya kaunti katika suala lolote linalohusiana na serikali ya kaunti iwapo litaombwa kufanya hivyo.

(7)Mahakama zingine zote ila Mahakama ya Juu Zaidi zitafuata maamuzi ya Mahakama ya Juu Zaidi.

(8)Mahakama ya Juu Zaidi itatunga sheria zitakazoongoza utekelezaji wa mamlaka yake.

(9)Sheria ya Bunge inaweza kutoa mwongozo zaidi kuhusu utendakazi wa Mahakama ya Juu Zaidi.

Isome ndani ya Sura ya Kumi →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho