Kamati za mamlaka ya utendaji katika kaunti
(1)Mamlaka ya utendaji katika kaunti yamepewa, na yatatekelezwa, na kamati za utendaji katika kaunti.
(2)Kamati ya utendaji katika kaunti inajumuisha—
(a)gavana wa kaunti na naibu gavana wa kaunti; na
(b)wanachama walioteuliwa na gavana wa kaunti, kwa idhini ya bunge la kaunti, kutoka miongoni mwa watu ambao sio wanachama wa bunge hilo.
(3)Idadi ya wanachama walioteuliwa kwa mujibu wa ibara ya (2)(b) haitazidi—
(a)thuluthi moja ya wanachama wa bunge la kaunti ikiwa bunge hilo lina chini ya wanachama thelathini; au
(b)kumi, ikiwa bunge lina wanachama thelathini au zaidi.
(4)Gavana wa kaunti na naibu gavana wa kaunti ndio afisa mkuu na naibu wa afisa mkuu wa kaunti, mtawalia.
(5)Wakati ambapo gavana wa kaunti hayupo, naibu gavana wa kaunti ndiye atakayehudumu kama gavana wa kaunti.
(6)Wanachama wa kamati ya utendaji katika kaunti wanawajibikia gavana wa kaunti katika utekelezaji wa majukumu na mamlaka yao.
(7)Ikiwa nafasi katika ofisi ya gavana itatokea, wanachama wa kamati ya utendaji katika kaunti walioteuliwa chini ya ibara ya (2) (b) hawatahudumu tena.