Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Moja · Serikali ya Ugatuzi

Kifungu cha 189

Kif.189

Ushirikiano kati ya serikali ya kitaifa na serikali za kaunti

(1)Serikali katika ngazi yoyote—

(a)iwapo ni serikali ya kaunti, serikali hiyo itatekeleza majukumu na mamlaka yake kwa namna inayoheshimu hadhi na uadilifu wa kitaasisi katika ngazi hiyo ya serikali, na kwa namna inayoheshimu hadhi ya kikatiba na taasisi za serikali katika ngazi hiyo nyingine ya serikali;

(b)itasaidia, itashirikiana na kushauriana na serikali katika ngazi hiyo nyingine, na ifaavyo, itatekeleza sheria za serikali iliyo katika ngazi hiyo nyingine; na

(c)itashauriana na serikali katika kiwango hicho kingine kwa madhumuni ya kubadilishana mawazo, kuratibia sera na utawala, na kuboresha uwezo wa kutekeleza majukumu.

(2)Serikali katika ngazi zote, na serikali tofauti katika ngazi ya kaunti, zitashirikiana katika kutekeleza majukumu na mamlaka yao, na kwa lengo hilo, zinaweza kubuni kamati na mamlaka ya pamoja.

(3)Katika mzozo wowote kati ya serikali, serikali hizo zitachukua hatua zote iwezekanavyo ili kutatua mzozo huo, ikijumuisha taratibu zilizotolewa chini ya sheria ya kitaifa.

(4)Sheria ya kitaifa itatoa taratibu za kutatua mizozo kati ya serikali kwa mbinu mbadala za kutatua mizozo zikiwemo kushauriana na upatanishi.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Moja →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho