Ustahiki katika kuchaguliwa kama mwakilishi wadi katika bunge la kaunti
(1)Isipokuwa kutostahiki chini ya ibara ya (2),mtu anastahiki kuchaguliwa kama mwakilishi wadi katika bunge la kaunti ikiwa mtu huyo—
(a)amesajiliwa kama mpiga kura;
(b)anatosheleza mahitaji yoyote ya kielimu, ya kimaadili na ya uadilifu ambayo yanahitajika katika Katiba hii au katika Sheria ya Bunge; na
(c)lazima awe—
(i)ameteuliwa na chama cha kisiasa; au
(ii)mgombea huru anayeungwa na angalau wapiga kura mia tano waliosajiliwa katika wadi husika.
(2)Mtu hastahiki kuchaguliwa kama mwakilishi wadi ikiwa mtu huyo—
(a)ni afisa wa Serikali au wa umma, isipokuwa mwakilishi wadi katika bunge la kaunti;
(b)amehudumu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka katika miaka mitano iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi.
(c)hajakuwa raia wa Kenya kwa angalau miaka kumi iliyopita kabla ya tarehe ya uchaguzi;
(d)hana akili timamu;
(e)amefilisika;
(f)anatumikia kifungo gerezani cha miezi sita au zaidi; au
(g)amepatikana kuwa, kulingana na sheria yoyote, ametumia vibaya mamlaka ya ofisi ya umma au kuwa amekiuka Sura ya Sita.
(3)Mtu hazuiliwi kugombea chini ya ibara ya (2) isipokuwa tu pale ambapo uwezekano wote wa rufaa au kukaguliwa kwa kifungo au uamuzi husika umekwisha.