Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Mbili · Fedha za Umma

Kifungu cha 203

Kif.203

Ugavi wenye usawa na sheria zingine za kifedha

(1)Vigezo vifuatavyo vitazingatiwa katika kutoa uamuzi kuhusu migao sawa iliyobainiwa chini ya Kifungu cha 202 na katika sheria zote za kitaifa zinazohusu serikali ya kaunti zinazotungwa kulingana na Sura hii—

(a)maslahi ya kitaifa;

(b)mgao wowote ambao lazima utolewe kwa mujibu wa deni la umma na majukumu mengine ya kitaifa;

(c)mahitaji ya serikali ya kitaifa yatakayoamuliwa kwa kutumia vigezo visivyoegemea upande wowote;

(d)hitaji la kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zina uwezo wa kutekeleza majukumu yaliyotolewa kwa serikali hizo;

(e)uwezo wa kifedha na ufanisi wa serikali za kaunti;

(f)maendeleo na mahitaji mengine ya serikali za kaunti;

(g)tofauti za kiuchumi miongoni mwa kaunti na kati ya kaunti na hitaji la kuzisawazisha;

(h)hitaji la kuchukua hatua sawazishi kwa sababu ya maeneo na vikundi vya watu wanyonge;

(i)hitaji la kuboresha uchumi katika kila kaunti na kutoa motisha ya kuboresha uwezo wa kuzalisha mapato katika kila kaunti;

(j)matamanio kuhusu mgao wa mapato ulio thabiti na unaoweza kutabirika;

(k)hitaji la wepesi katika kukabiliana na majanga na mahitaji mengine ya muda mfupi, kwenye misingi sawa ya vigezo visivyoegemea upande wowote.

(2)Katika kila mwaka wa fedha, mgao unaolingana na mapato yaliyozalishwa kitaifa ambao utatengewa serikali za kaunti hautakuwa chini ya asilimia kumi na tano ya mapato yote ambayo yalikusanywa na serikali ya kitaifa.

(3)Kiasi cha fedha zilizotajwa katika ibara ya (2) zitahesabiwa kwenye msingi wa akaunti zilizokaguliwa hivi majuzi kuhusu mapato yaliyokusanywa, kama ilivyoidhinishwa na Bunge la Kitaifa.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Mbili →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho