Utekelezaji wa haki na uhuru wa kimsingi
(1)Ni wajibu wa kimsingi wa Serikali na kila idara ya Serikali kuzingatia, kuheshimu, kulinda, kukuza na kutimiza haki na uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki.
(2)Serikali itachukua hatua za kisheria, kisera na nyinginezo ikijumuisha uwekaji wa viwango ili kufanikisha upatikanaji endelevu wa haki hizo kama ilivyohakikishwa chini ya Kifungu cha 43.
(3)Ni wajibu wa idara zote za Serikali na maafisa wote wa umma kushughulikia mahitaji ya makundi ya watu walio hatarini katika jamii, ikijumuisha wanawake, wazee katika jamii, watu wenye ulemavu, watoto, vijana na jamii za walio wachache au zilizotengwa, pamoja na jamii fulani za kikabila, kidini au kitamaduni.
(4)Serikali itatunga na kutekeleza sheria ili kutimiza wajibu wake wa kimataifa kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kimsingi.