Matumizi ya ziada
(1)Kwa kuzingatia ibara ya (2) hadi (4), serikali ya kitaifa inaweza kutumia fedha ambazo hazijaidhinishwa ikiwa—
(a)kiasi kilichotengwa kwa madhumuni yoyote chini ya Sheria Kuhusu Matumizi ya Fedha hakitoshi au hitaji limetokea la matumizi ambayo hayakuwa yamekadiriwa na kuidhinishwa na Sheria hiyo; au
(b)fedha zimetolewa kutoka kwenye Hazina ya Dharura.
(2)Idhini ya Bunge kuhusu matumizi yoyote chini ya Kifungu hiki itafuatiliwa katika muda wa miezi miwili baada ya fedha kutolewa kwa mara ya kwanza, lakini kwa kuzingatia ibara ya (3).
(3)Ikiwa Bunge halitakuwa na vikao katika muda uliobainishwa katika ibara ya (2), au lina vikao lakini liende mapumzikoni kabla ya idhini kutolewa, idhini hiyo itafuatiliwa katika muda wa wiki mbili baada ya kikao chake kitakachofuata.
(4)Bunge la Kitaifa litakapokuwa limeidhinisha matumizi chini ya ibara ya (2), Mswada kuhusu matumizi ya fedha utawasilishwa ili kuidhinisha matumizi ya fedha.
(5)Katika mwaka wowote wa kifedha, serikali ya kitaifa haiwezi kutumia fedha chini ya Kifungu hiki, kwa kiasi kinachozidi asilimia kumi ya fedha zilizotengwa na Bunge kwa mwaka huo, isipokuwa Bunge liidhinishe asilimia ya juu kuliko asilimia kumi, katika hali maalum.