Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Mbili · Fedha za Umma

Kifungu cha 230

Kif.230

Tume ya Mishahara na Malipo

(1)Tume ya Mishahara na Malipo imebuniwa.

(2)Tume ya Mishahara na Malipo inajumuisha watu wafuatao watakaoteuliwa na Rais—

(a)mwenyekiti;

(b)watu walioteuliwa na mashirika yafuatayo, miongoni mwa watu ambao sio wanachama au wafanyakazi katika mashirika hayo—

(i)Tume ya Huduma za Bunge;

(ii)Tume ya Huduma za Umma;

(iii)Tume ya Huduma za Mahakama;

(iv)Tume ya Huduma kwa Walimu;

(v)Tume ya Kitaifa ya Huduma za Polisi;

(vi)Baraza la Ulinzi; na

(vii)Seneti, kwa niaba ya serikali za kaunti;

(c)mtu mmoja aliyeteuliwa na—

(i)shirika linalowakilisha vyama vya wafanyakazi;

(ii)shirika linalowakilisha waajiri; na

(iii)baraza la pamoja la mashirika ya kitaaluma kulingana na sheria;

(d)mtu mmoja aliyeteuliwa na—

(i)Waziri anayewajibikia masuala ya fedha; na

(ii)Mwanasheria Mkuu; na

(e)mtu aliye na uzoefu katika usimamizi wa wafanyakazi katika huduma za umma, aliyeteuliwa na Waziri anayesimamia huduma za umma.

(3)Makamishna waliotajwa katika ibara ya (1) (d) na (e) hawatakuwa na uwezo wa kupiga kura.

(4)Mamlaka na majukumu ya Tume ya Mishahara na Malipo yatakuwa—

(a)kuweka viwango vya mishahara na marupurupu ya maafisa wote wa Serikali, na kukagua mishahara na marupurupu hayo; na

(b)kushauri serikali ya kitaifa na serikali za kaunti kuhusu mishahara na marupurupu ya maafisa wote wengine wa serikali.

(5)Katika kutekeleza majukumu yake, Tume hiyo itazingatia kanuni zifuatazo—

(a)hitaji la kuhakikisha kuwa bili ya kijumla ya malipo kwa umma ni endelevu kifedha;

(b)hitaji la kuhakikisha kwamba huduma za umma zina uwezo wa kuwavutia na kudumisha wahudumu walio na ujuzi unaohitajika ili kutekeleza majukumu yao;

(c)hitaji la kutambua uzalishaji na utendakazi; na

(d)uwazi na usawa.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Mbili →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho