Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Nne · Usalama wa Kitaifa

Kifungu cha 241

Kif.241

Kuundwa kwa Baraza la Ulinzi na Vikosi vya Ulinzi

(1)Vikosi vya Ulinzi wa Kenya vimebuniwa.

(2)Vikosi hivyo vya Ulinzi vinajumuisha—

(a)Jeshi la Kenya la Nchi Kavu;

(b)Jeshi la Kenya la Anga; na

(c)Jeshi la Kenya la Wanamaji.

(3)Vikosi vya Ulinzi—

(a)vina jukumu la ulinzi wa uhuru na mamlaka ya mipaka ya Jamhuri;

(b)vitasaidia na kushirikiana na mashirika mengine katika hali za dharura au majanga, na kutoa ripoti kwa Bunge la Kitaifa wakati wowote yanapotekeleza shughuli kama hizo; na

(c)vinaweza kupelekwa ili kurejesha amani katika sehemu yoyote nchini Kenya inayokumbwa na machafuko, lakini tu kwa idhini ya Bunge la Kitaifa.

(4)Uongozi katika Vikosi yya Ulinzi utaonyesha utofauti wa kimaeneo na kijamii wa watu wa Kenya.

(5)Baraza la Ulinzi limebuniwa.

(6)Baraza litajumuisha—

(a)Waziri anayewajibika kuhusu ulinzi, ambaye ndiye mwenyekiti;

(b)Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya;

(c)makamanda watatu wa vikosi vya ulinzi; na

(d)Katibu Mkuu katika wizara inayowajibika kuhusu ulinzi.

(7)Baraza––

(a)linawajibika katika sera ya kijumla, udhibiti na usimamizi wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya; na

(b)hutekeleza majukumu mengine yoyote yaliyotolewa kwa mujibu wa sheria ya kitaifa.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Nne →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho