Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Sita

Marekebisho ya Katiba Hii

Jinsi Katiba hii inavyoweza kurekebishwa, na Bunge au na wananchi.

Vifungu 255–257 · vifungu 3

Kif.255

Marekebisho ya Katiba Hii

(1)Pendekezo la marekebisho ya Katiba hii litatekelezwa kulingana na Kifungu cha 256 au 257, na kupitishwa kulingana na ibara ya (2) katika kura ya maamuzi, ikiwa marekebisho hayo yanahusu suala lolote kati ya masuala yafuatayo—

(a)ukuu wa Katiba hii;

(b)teritori ya Kenya;

(c)mamlaka makuu ya wananchi;

(d)maadili ya kitaifa, kanuni za kiutawala zilizotajwa katika Kifungu cha 10 (2) (a) hadi (d);

(e)Sheria za Haki;

(f)muhula wa kuhudumu katika ofisi ya Rais;

(g)uhuru wa Kitengo cha Mahakama na tume na ofisi huru zinazorejelewa katika Sura ya Kumi na Tano;

(h)majukumu ya Bunge;

(i)malengo, kanuni na muundo wa serikali ya ugatuzi; au

(j)vifungu katika Sura hii.

(2)Pendekezo la marekebisho litapitishwa kwa kura ya maamuzi chini ya ibara ya (1) ikiwa—

(a)angalau asilimia ishirini ya wapiga kura waliosajiliwa katika angalau nusu ya idadi ya kaunti itapiga kura katika kura ya maamuzi; na

(b)marekebisho hayo yanaungwa mkono na idadi kubwa ya wananchi wanaopiga kura katika kura ya maamuzi.

(3)Marekebisho katika Katiba hii ambayo hayahusiani na masuala yaliyofafanuliwa katika ibara ya (1) yatapitishwa—

(a)na Bunge, kulingana na Kifungu cha 256; au

(b)na wananchi pamoja na Bunge, kulingana na Kifungu cha 257.

Kif.256

Marekebisho kwa njia ya mapendekezo ya bunge

(1)Mswada wa kurekebisha Katiba hii—

(a)unaweza kuwasilishwa katika Kitengo chochote cha Bunge;

(b)haupaswi kuangazia suala lolote lingine isipokuwa yale yanayotokana na marekebisho ya sheria katika Mswada huo;

(c)hautawasilishwa ili kusomwa kwa mara ya pili katika Kitengo chochote cha Bunge, katika muda wa siku tisini baada ya kusomwa kwa Mswada huo kwa mara ya kwanza katika Kitengo hicho cha Bunge; na

(d)utakuwa umepitishwa na Bunge kila Kitengo cha Bunge kitakapopitisha Mswada huo katika usomaji wa Mswada huo kwa mara ya pili na tatu, kwa idadi isiyopungua thuluthi mbili ya wanachama wote katika Kitengo hicho.

(2)Bunge litatangaza kuhusu Mswada wowote wa kurekebisha Katiba hii, na kuwezesha mjadala wa umma kuhusiana na Mswada huo.

(3)Baada ya Bunge kupitisha Mswada wa kurekebisha Katiba hii, Maspika wa Vitengo vyote viwili vya Bunge watawasilishia Rais, kwa pamoja—

(a)Mswada huo, ili kuidhinishwa na kuchapishwa; na

(b)cheti kinachothibitisha kwamba Mswada huo umepitishwa na Bunge kulingana na Kifungu hiki.

(4)Kwa kuzingatia ibara ya (5), Rais ataidhinisha Mswada huo na kuufanya uchapishwe katika muda wa siku thelathini baada ya Mswada huo kupitishwa na Bunge.

(5)Ikiwa Mswada wa kurekebisha Katiba hii unapendekeza marekebisho yanayohusiana na suala lililotajwa katika Kifungu cha 255 (1)—

(a)kabla ya kuuidhinisha Mswada huo, Rais ataiomba Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kuandaa kura ya maamuzi ya kitaifa katika muda wa siku tisini ili Mswada huo uidhinishwe; na

(b)katika muda wa siku thelathini baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka kumthibitishia Rais kwamba Mswada huo umepitishwa kulingana na Kifungu cha 255 (2), Rais ataidhinisha Mswada huo na kuufanya uchapishwe.

Kif.257

Marekebisho kwa njia ya mapendekezo ya wananchi wengi

(1)Marekebisho ya Katiba hii yanaweza kupendekezwa kupitia kwa juhudi za wengi ikiwa angalau wapiga kura milioni moja waliosajiliwa watatia saini kwenye pendekezo hilo.

(2)Marekebisho ya Katiba hii yanayoanzishwa kupitia juhudi za wananchi wengi yanaweza kuchukua muundo wa pendekezo la kijumla au Mswada ulioandaliwa.

(3)Ikiwa pendekezo la wananchi wengi litachukua muundo wa pendekezo la kijumla, wanaoongoza pendekezo hilo wataliandaa liwe Mswada rasimu.

(4)Wanaoongoza pendekezo hilo la wananchi wengi watawasilisha rasimu ya Mswada pamoja na saini zinazounga mkono rasimu hiyo kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ambayo itathibitisha kwamba pendekezo hilo linaungwa mkono na angalau wapiga kura milioni moja waliosajiliwa.

(5)Ikiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itaridhika kwamba pendekezo hilo limetimiza mahitaji ya Kifungu hiki, Tume itawasilisha pendekezo hilo kwa kila bunge la kaunti ili kujadiliwa katika muda wa miezi mitatu baada ya tarehe ya kuwasilishwa na Tume hiyo.

(6)Ikiwa bunge la kaunti litaidhinisha rasimu ya Mswada huo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya tarehe ya kuwasilishwa na Tume, spika wa bunge la kaunti atawasilisha nakala ya rasimu ya Mswada kwa Maspika wa Vitengo vyote viwili vya Bunge, pamoja na cheti kinachothibitisha kwamba bunge la kaunti limeidhinisha rasimu ya Mswada huo.

(7)Ikiwa rasimu ya Mswada imeidhinishwa na idadi kubwa ya mabunge ya kaunti, rasimu hiyo itawasilishwa Bungeni bila kuchelewa.

(8)Mswada chini ya Kifungu hiki umepitishwa na Bunge ikiwa umeungwa mkono na idadi kubwa ya wanachama wa kila Kitengo cha Bunge.

(9)Ikiwa Bunge litapitisha Mswada huo, utawasilishwa kwa Rais ili kuidhinishwa kulingana na Vifungu vya 256 (4) na (5).

(10)Ikiwa mojawapo ya Vitengo vya Bunge kitakosa kupitisha Mswada huo, au Mswada huo unahusu suala lililotajwa katika kifungu cha 255 (1), marekebisho yaliyopendekezwa yatawasilishwa kwa wananchi katika kura ya maamuzi.

(11)Kifungu cha 255 (2) kitatumika, kwa kuzingatia mabadiliko yoyote yatakayohitajika, katika kura ya maamuzi chini ya ibara ya (10).

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho