Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Sita

Uongozi na Uadilifu

Viwango ambavyo kila afisa wa Serikali lazima afikie.

Vifungu 73–80 · vifungu 8

Kif.73

Wajibu wa uongozi

(1)Mamlaka yaliyotolewa kwa afisa wa Serikali—

(a)ni amana ya umma inayopaswa kutekelezwa kwa njia ambayo—

(i)inaambatana na madhumuni na malengo ya Katiba hii;

(ii)inaonyesha heshima kwa watu;

(iii)inaleta sifa njema kwa taifa na heshima kwa ofisi hiyo; na

(iv)inakuza imani ya umma katika uadilifu wa ofisi hiyo; na

(b)inampa afisa huyo wa Serikali jukumu la kuwahudumia watu, na wala sio mamlaka ya kuwatawala.

(2)Kanuni zinazotoa mwongozo katika uongozi na uadilifu zinajumuisha—

(a)uteuzi kwenye misingi ya uadilifu, ustadi kazini na kufaa kwa mtu huyo, au kuchaguliwa katika uchaguzi huru na wa haki;

(b)kutopendelea upande wowote katika kufanya maamuzi na katika kuhakikisha kwamba maamuzi hayo hayatokani na mapendeleo ya kindugu, upendeleo, nia zingine zozote mbaya au vitendo vya kifisadi;

(c)huduma ya kujitolea kwenye misingi ya manufaa kwa umma, inayoonyeshwa kwa—

(i)uaminifu katika utekelezaji wa majukumu ya umma; na

(ii)kutangaza maslahi ya kibinafsi yanayoweza kugongana na wajibu wake kwa umma;

(d)uwajibikaji kwa umma kuhusu maamuzi na hatua zinazochukuliwa; na

(e)nidhamu na kujitolea katika kuwahudumia watu.

Kif.74

Kiapo cha uaminifu cha Maafisa wa Serikali

Kabla ya kuchukua hatamu katika ofisi ya serikali, au kutekeleza majukumu yoyote katika ofisi ya Serikali, mtu aliyechaguliwa au kuteuliwa ataapa au kukiri kwa uthibitisho kuwa atawajibikia ofisi hiyo, kwa kuzingatia njia iliyopendekezwa na Ambatisho la Tatu, au chini ya Sheria ya Bunge.

Kif.75

Mienendo ya maafisa wa Serikali

(1)Afisa wa Serikali atakuwa na mienendo inayokubalika, katika maisha yake ya kirasmi, katika maisha ya kibinafsi, au anapotangamana na watu wengine, na kwa njia ambayo inaepuka—

(a)mgongano wowote kati ya maslahi ya kibinafsi na majukumu rasmi au ya umma;

(b)kupendelea maslahi ya kibinafsi badala ya maslahi ya umma; au

(c)kudunisha hadhi ya ofisi ambayo afisa huyo anasimamia.

(2)Mtu anayekiuka sehemu ya (1), au Kifungu cha 76, 77 au 78 (2)—

(a)atawekwa chini ya taratibu za kinidhamu zinazotumika katika ofisi inayohusika;

(b)kulingana na taratibu za kinidhamu zinazorejelewa katika aya ya (a), anaweza kuachishwa kazi au kwa njia nyingine kuondolewa ofisini.

(3)Mtu ambaye ameachishwa kazi au vinginevyo kuondolewa ofisini kwa kukiuka masharti yaliyotajwa katika sehemu ya (2) atapigwa marufuku dhidi ya kushikilia ofisi yoyote nyingine ya Serikali.

Kif.76

Uadilifu wa kifedha wa maafisa wa Serikali

(1)Zawadi au mchango wowote kwa afisa wa Serikali katika shughuli rasmi au za umma, utakuwa mchango au zawadi kwa Jamhuri na itakabidhiwa Serikali isipokuwa kuwe na Sheria ya Bunge itakayobat -ilisha hayo.

(2)Afisa wa Serikali—

(a)hatamiliki akaunti ya benki nje ya Kenya isipokuwa kulingana na Sheria ya Bunge; au

(b)hataomba au kukubali mkopo au manufaa ya kibinafsi katika hali zinazotatiza uadilifu wake.

Kif.77

Udhibiti katika shughuli za maafisa wa Serikali

(1)Afisa wa Serikali anayehudumu wakati wote hatashiriki katika ajira nyingine yenye mapato.

(2)Afisa yeyote wa Serikali aliyeteuliwa hatahudumu katika ofisi ya chama cha kisiasa.

(3)Afisa wa Serikali aliyestaafu na anayepokea malipo ya uzeeni kutoka kwenye fedha za umma, hatahudumu katika zaidi ya nyadhifa mbili zilizo na mshahara kwa wakati mmoja kama mwenyekiti, mkurugenzi au mfanyakazi wa—

(a)kampuni inayomilikiwa au kudhibitiwa na Serikali; au

(b)idara ya Serikali.

(4)Afisa wa Serikali aliyestaafu hatapokea malipo kutoka kwa fedha za umma isipokuwa kama ilivyobainishwa katika sehemu ya (3).

Kif.78

Uraia na uongozi

(1)Hakuna mtu anayepaswa kuchaguliwa au kuteuliwa katika ofisi ya Serikali ikiwa si raia wa Kenya.

(2)Afisa wa Serikali au afisa aliye katika vikosi vya ulinzi hatakuwa na uraia wa nchi mbili.

(3)Sehemu za (1) na (2) hazitumiki kwa—

(a)majaji na wanachama wa tume; au

(b)mtu yeyote ambaye amekuwa raia wa nchi nyingine kupitia kwa utekelezaji wa sheria ya nchi hiyo, na ambaye hana uwezo wa kuondoa uraia huo.

Kif.79

Sheria ya kuundwa kwa tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi

Bunge litatunga sheria ya kubuniwa kwa tume huru ya maadili na kupambana na ufisadi, ambayo itakuwa na hadhi na mamlaka sawa na tume iliyo chini ya Sura ya Kumi na Tano, kwa madhumuni ya kuhakikisha utimizaji na utekelezaji wa masharti ya Sura hii.

Kif.80

Sheria zinazohusu uongozi

Bunge litatunga sheria—

(a)itakayotoa taratibu na mikakati ya utekelezaji wa Sura hii kwa njia ifaayo;

(b)itakayopendekeza adhabu za ziada, kando na zile zinazorejelewa katika Kifungu cha 75, ambazo zinaweza kuamriwa kwa sababu ya ukiukaji wa Sura hii;

(c)itakayotoa mwongozo wa utekelezaji wa Sura hii kwa maafisa wa umma, pamoja na marekebisho yanayohitajika; na

(d)Itakayotoa mwongozo wowote mwingine unaohitajika ili kuhakikisha ukuzaji wa kanuni za uongozi na uadilifu zilizotajwa katika Sura hii, na utekelezaji wa Sura hii.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho