Katiba ya Kenya, 2010
Ambatisho la Tatu · Vifungu vya 74, 141 (3), 148 (5) na 152(4)
Viapo na Uthibitsho wa Kitaifa
Kiapo Au Uthibitisho Rasmi wa Uaminifu wa Rais/Rais Anayehudumu kwa Muda Mfupi na wa Naibu wa Rais
Mimi,.................................................................................... , nikifahamu kikamilifu kuhusu mwito mkuu ambao ninatumikia kama Rais/Rais wa Muda Mfupi/ Naibu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya, ninaapa/ ninatoa uthibitisho rasmi kwamba nitakuwa mwaminifu na kutoa uaminifu wa kweli kwa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitaitii, nitaihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba hii ya Kenya, kama ilivyowekwa kwa sheria, na sheria zote zinginezo za Jamhuri; na kwamba nitalinda na kukuza ukuu, uadilifu na hadhi ya wananchi wa Kenya. (Iwapo ni kiapo–– Ee Mungu nisaidie.)
Kiapo Au Uthibitisho Rasmi wa Utendakazi katika Ofisi ya Rais/Rais wa Muda Mfupi
Mimi,............................................................, ninaapa/ninatoa uthibitisho kwamba kwa kweli na bidii nitawahudumia wananchi na Jamhuri ya Kenya katika ofisi ya Rais/ Rais wa Muda Mfupi wa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatekeleza majukumu yangu na utendakazi wangu kwa bidii katika Ofisi ya Rais/ Rais wa Muda Mfupi wa Jamhuri ya Kenya; na nitawatendea haki wote kulingana na Katiba hii, ilivyowekwa kisheria, na kwa sheria za Kenya, bila woga, upendeleo, upendo au nia mbaya. (Iwapo ni kiapo–– Ee Mungu nisaidie.)
Kiapo Au Uthibitisho Rasmi wa Utendakazi kwa Naibu Rais
Mimi,............................................................, ninaapa/ ninatoa Rasmi kuwa nitawatumikia wananchi na Jamhuri ya Kenya kila wakati kwa ukweli na bidii katika ofisi ya Naibu wa Rais wa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatekeleza majukumu yangu na kutenda kazi kwa bidii katika ofisi hiyo, kwa kadri ya uwezo wangu; kwamba kwa wakati wote ninapohitajiwa nitatoa ushauri wangu kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya; kwamba nitawatendea haki wote bila woga, upendeleo, upendo au nia mbaya na kwamba sitafichua kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo maswala nitakayoyafahamu katika utekelezaji wa majukumu yangu na ambayo ninapaswa kuyaweka kwa usiri. (Iwapo ni kiapo–– Ee Mungu nisaidie.)
Kiapo Au Uthibitisho Rasmi wa Utendakazi kwa Waziri
Mimi,............................................................, nikiwa nimeteuliwa kama Waziri nchini Kenya, ninaapa/ninatoa uthibitisho rasmi kwamba nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Kenya kila wakati; kwamba nitaitii, nitaihifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba hii ya Kenya na sheria zote zingine za Jamhuri; kwamba nitawatumikia wananchi wa Jamhuri ya Kenya kwa ukweli katika Ofisi ya Waziri; kwamba ninaahidi kuhudumu kama Waziri kwa njia ya heshima na hadhi; kwamba nitakuwa mshauri mwaminifu na wa kweli wa Rais kwa madhumuni ya usimamizi bora katika maswala ya umma katika Jamhuri ya Kenya; kwamba sitafichua kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo maswala nitakayoyafahamu katika utekelezaji wa majukumu yangu na ambayo ninapaswa kuyaweka kwa usiri isipokuwa itakapohitajika nifichue maswala hayo katika utekelezaji wa majukumu yangu kama Waziri; na kwamba nitatekeleza majukumu ya ofisi yangu kwa ufahamu na kadri ya uwezo wangu.
(Iwapo ni kiapo–– Ee Mungu nisaidie.).
Kiapo Au Uthibitisho Rasmi wa Utendakazi kwa Katibu wa Baraza la Mawaziri/Katibu Mkuu
Mimi,............................................................, nikiwa ninahitajiwa ili kutekeleza majukumu ya Katibu wa Baraza la Mawaziri/Katibu Mkuu, ninaapa/ninatoa uthibitisho rasmi kwamba, isipokuwa kwa idhini ya Rais, sitafichua kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo, hali na yaliyomo katika kikao, shughuli au hati yoyote ya Baraza la Mawaziri ambayo ninapaswa kuweka kwa usiri isipokuwa itakapohitajika nifichue maswala hayo katika utekelezaji wa majukumu yangu kama Katibu wa Baraza la Mawaziri/Katibu Mkuu. (Iwapo ni kiapo–– Ee Mungu nisaidie.
Viapo kwa Jaji Mkuu /Rais wa Mahakama ya Juu Zaidi, Majaji wa Mahakama ya Juu Zaidi, Majaji wa Mahakama ya Rufaa na Majaji wa Mahakama Kuu.
Mimi,............................................................, (Jaji Mjuu/ Rais wa Mahakama ya Juu Zaidi, jaji wa Mahakama ya Juu Zaidi, jaji wa Mahakama ya Rufaa, jaji wa Mahakama Kuu) nina (apa kwa jina la Mwenyezi Mungu)/(ninatoa uthibitisho rasmi) kutumikia wananchi na Jamhuri ya Kenya na kutekeleza haki bila mapendeleo kulingana na Katiba hii na ilivyowekwa kisheria, na sheria na desturi za Jamhuri, bila woga wowote, upendeleo, ubaguzi, upendo, chuki, au mvuto wowote wa kisiasa, kidini, ama ushawishi wowote mwingine. Katika kutekeleza majukumu ya kisheria ambayo nimepewa, kwa uwezo wangu wote, na kwa wakati wote, nitailinda, nitaitekeleza na kuitetea Katiba hii kwa madhumuni ya kulinda hadhi na heshima ya kitengo cha mahakama na mfumo wa mahakama wa Kenya na nitakuza haki, uhuru, ustadi na uadilifu ndani yake. (Ee Mungu nisaidie.)
Kiapo/Uthibitisho kwa Mwanachama wa Bunge (Seneti/ Bunge la Kitaifa)
I,............................................................, nikiwa nimechaguliwa kama mwanachama wa Seneti/Bunge la Kitaifa ninaapa (Kwa jina la Mwenyezi Mungu) (ninatoa uthibitisho rasmi) kwamba nitakuwa mwaminifu na kuwa na imani ya kweli katika Wananchi na Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatii, kuheshimu, kutetea, kulinda na kuhifadhi Katiba ya Jamhuri ya Kenya; na kwamba nitatekeleza majukumu ya mwanachama wa Bunge kwa uaminifu na uangalifu. (Ee Mungu nisaidie).
Kiapo cha Spika/Naibu wa Spika wa Seneti/Bunge la Kitaifa
Mimi,............................................................, nikiwa nimechaguliwa kama Spika/ Naibu wa Spika wa Seneti/Bunge la Kitaifa ninaapa (kwa jina la Mwenyezi Mungu)
(ninatoa uthibitisho rasmi) kwamba nitakuwa mwaminifu kikweli kwa wananchi na Jamhuri ya Kenya; kwamba nitatekeleza kwa uaminifu na uangalifu majukumu yangu kama Spika/Naibu wa Spika wa Seneti/Bunge la Kitaifa; kwamba nitatii, nitaheshimu, nitatea, nitahifadhi, nitalinda na kuitetea Katiba hii ya Jamhuri ya Kenya; na kwamba nitatenda haki kwa watu wote kulingana na Katiba hii ya Kenya na sheria na desturi za Bunge bila woga au upendeleo, upendo au chuki (Ee Mungu nisaidie).