Katiba ya Kenya, 2010
Ambatisho la Nne · Kifungu cha 185 (2), 186 (1) na 187 (2)
Ugawaji wa Majukumu Kati ya Serikali ya Kitaifa na Serikali za Kaunti
Sehemu ya 1—Serikali ya Kitaifa
(1)Maswala ya kigeni, sera ya kigeni na biashara ya kimataifa.
(2)Matumizi ya maji ya kimataifa na rasilimali za maji.
(3)Uhamiaji na uraia.
(4)Uhusiano kati ya dini na serikali.
(5)Sera ya lugha na ukuzaji wa lugha rasmi na lugha za kiasili.
(6)Ulinzi wa kitaifa na matumizi ya huduma za ulinzi za kitaifa.
(7)Huduma za polisi, ikijumuisha—
(a)uwekaji viwango vya kuajiri, mafunzo kwa polisi na matumizi ya huduma za polisi;
(b)sheria ya jinai; na
(c)huduma za marekebisho.
(8)Mahakama.
(9)Sera ya kitaifa ya uchumi na mipango.
(10)Sera ya fedha, sarafu, benki (ikijumuisha benki kuu) kusajiliwa na kudhibitiwa kwa shughuli za benki, bima na mashirika ya kifedha.
(11)Takwimu za kitaifa na data kuhusu idadi ya watu, uchumi na jamii kwa jumla.
(12)Haki za uvumbuzi.
(13)Viwango vya utendakazi.
(14)Ulinzi wa watumiaji wa bidhaa na huduma, ikijumuisha viwango vya usalama wa kijamii na mipango ya kitaalamu kuhusu kustaafu.
(15)Sera ya elimu, viwango, mitaala, mitihani, na utoaji wa hati za kuidhinisha vyuo vikuu.
(16)Vyuo Vikuu, taasisi za mafunzo na taasisi zinginezo za utafiti na masomo ya juu na shule za msingi, elimu maalum, shule za upili na vyuo vya elimu maalum.
(17)Ukuzaji wa michezo na elimu ya michezo.
(18)Uchukuzi na mawasiliano, ikijumuisha hasa—
(a)usafiri wa barabarani;
(b)ujenzi na matumizi ya barabara kuu za kimataifa;
(c)viwango vya ujenzi na uhifadhi wa barabara zingine zitakazojengwa na kaunti;
(d)reli;
(e)mabomba ya mafuta;
(f)usafiri wa baharini;
(g)usafiri wa ndege;
(h)usafiri wa angani;
(i)huduma za posta;
(j)mawasiliano ya simu; na
(k)utangazaji wa redio na runinga.
(19)Kazi za umma za kitaifa.
(20)Sera ya makazi.
(21)Kanuni za kijumla za mipango ya ardhi na uratibu wa mipango katika kaunti.
(22)Ulinzi wa mazingira na mali-asili kwa madhumuni ya kubuni mfumo wa maendeleo endelevu, ikijumuisha hasa—
(a)uvuvi, uwindaji na ukusanyaji;
(b)ulinzi wa wanyama na wanyama pori;
(c)ulinzi wa maji, kuhifadhi maji yanayobaki, uhandisi unaohusu maji na usalama wa mabwawa; na
(d)sera ya kawi.
(23)Vituo vya afya vya rufaa vya kitaifa.
(24)Usimamizi katika majanga
(25)Minara ya zamani ya kihistoria yenye umuhimu wa kitaifa.
(26)Uchaguzi wa kitaifa.
(27)Sera ya afya.
(28)Sera ya Kilimo.
(29)Sera ya utabibu wa mifugo.
(30)Sera ya kawi pamoja na nguvu za umeme, gesi, na udhibiti wa kawi.
(31)Ukuzaji wa uwezo wa utendakazi na usaidizi wa kiufundi katika kaunti.
(32)Uwekezaji wa umma.
(33)Uchezaji kamari wa kitaifa, makasino na aina mbalimbali za uchezaji kamari.
(34)Sera ya utalii na maendeleo.
Sehemu ya 2—Serikali za Kaunti
Majukumu na mamlaka ya kaunti ni—
(35)Kilimo, ikijumuisha—
(a)kilimo cha mimea na wanyama;
(b)viwanja vya kuuzia mifugo;
(c)vichinjio vya kaunti;
(d)udhibiti wa magonjwa ya mimea na wanyama; na
(e)uvuvi.
(36)Huduma za afya za kaunti ikijumuisha hasa—
(a)vituo vya afya vya kaunti na famasia;
(b)huduma za ambulensi;
(c)ukuzaji wa afya ya kimsingi;
(d)kutoa leseni na kusimamia shughuli za kuuza vyakula kwa umma;
(e)huduma za matibabu ya wanyama (isipokuwa udhibiti wa taaluma hii);
(f)makaburi, ukumbi wa matanga na tanuu za kuchomea maiti; na
(g)uondoaji taka, maeneo ya kutupa taka na utupaji taka.
(37)Kudhibiti uchafuzi wa hewa, uchafuzi wa mazingira kupitia kwa kelele, usumbufu mwingine kwa umma na utangazaji wa nje.
(38)Shughuli za kitamaduni, burudani za umma na huduma za umma ikijumuisha—
(a)mchezo wa kamari, makasino na aina nyingine ya kucheza kamari;
(b)mashindano ya mbio;
(c)utoaji leseni kwa uuzaji wa pombe;
(d)Majumba ya sinema;
(e)maonyesho ya video na ukodishaji;
(f)maktaba;
(g)majumba ya makumbusho;
(h)michezo na shughuli za kitamaduni na vifaa; na
(i)bustani za kaunti, fuo na vifaa vya burudani.
(39)uchukuzi katika kaunti, ikijumuisha—
(a)barabara za kaunti;
(b)taa za barabarani;
(c)usafiri na uegeshaji;
(d)usafiri wa barabarani wa umma ; na
(e)vivuko na bandari, lakini bila usimamizi wa usafirishaji wa kitaifa na kimataifa na shughuli zinazohusiana na usafirishaji huo.
(40)Udhibiti na hali ya wanyama, ikijumuisha—
(a)utoaji leseni kuhusu ufugaji na matumizi ya mbwa; na
(b)Nyenzo za kuhifadhi, kutunza na kuzika wanyama.
(41)Maendeleo na udhibiti wa biashara, ikijumuisha—
(a)masoko;
(b)leseni za biashara (bila kujumuisha udhibiti wa taaluma);
(c)usawa katika shughuli za kibiashara;
(d)utalii wa humu nchini; na
(e)vyama vya ushirika.
(42)Mipango na maendeleo ya kaunti, ikijumuisha—
(a)takwimu;
(b)upimaji wa ardhi na utengenezaji wa ramani;
(c)mipaka na uwekaji nyua;
(d)makazi; na
(e)uunganishaji wa nguvu za umeme na gesi na udhibiti wa kawi.
(43)Elimu ya chekechea, vyuo vya kiufundi vijijini, vituo vya utengenezaji wa vyombo vya kinyumbani na vituo vya utunzaji wa watoto.
(44)Utekelezaji wa sera maalum za serikali ya kitaifa kuhusu mali-asili na uhifadhi wa mazingira, ikijumuisha—
(a)uhifadhi wa udongo na maji; na
(b)misitu.
(45)Huduma za kazi kwa umma katika kaunti ikijumuisha—
(a)mfumo wa usimamizi wa maji ya tufani katika sehemu za majengo; na
(b)huduma za maji na usafi.
(46)Huduma za kuzima moto, na udhibiti wa majanga.
(47)Udhibiti wa dawa za kulevya na ponografia.
(48)Kuhakikisha na kusimamia ushiriki wa jamii na sehemu za mashambani katika utawala wa viwango hivyo vya mashinani na kuzisaidia jamii pamoja na maeneo hayo kukuza uwezo wa kiusimamizi ili kuwezesha utekelezaji mwema wa mamlaka na majukumu na kushiriki katika utawala wa mashinani.