Katiba ya Kenya, 2010

Ambatisho la Sita · Kifungu cha 262

Vifungu vya Mpito na Vitakavyotumiwa Katiba Hii Itakapoanza Kutumika

Sehemu ya 1—Vifungu vya Kijumla

1. Ufasiri

Katika Ambatisho hili, isipokuwa muktadha uhitaji vinginevyo—

(a)“Tume ya Mipaka” inamaanisha Tume Huru ya Muda ya Mipaka;

(b)“Tume ya Uchaguzi” inamaanisha Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi;

(c)“katiba ya awali” inamaanisha Katiba iliyotumika kabla ya Katiba hii kuanza kutumika.

2. Utekelezaji wa vifungu vya Katiba hii Kusitishwa

(1)Kutekelezwa kwa vifungu vifuatavyo vya Katiba hii kumesitishwa hadi tangazo la mwisho la matokeo yote ya uchaguzi wa kwanza wa Bunge chini ya Katiba hii––

(a)Sura ya Saba, isipokuwa kwamba vifungu vya sura hii vitatumika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya Katiba hii;

(b)Sura ya Nane, isipokuwa kwamba vifungu vya Sura hiyo vinavyohusiana na uchaguzi wa Bunge la Kitaifa na la Seneti, vitatumika katika uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya Katiba hii; na

(c)Vifungu vya 129 hadi 155 vya Sura ya Tisa, isipokuwa vifungu vya Sura hiyo vinavyohusiana na uchaguzi wa Rais, vitatumika katika uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya Katiba hii.

(2)Utekelezaji wa vifungu vya Katiba hii vinavyohusiana na serikali ya ugatuzi, ikijumuisha Kifungu cha 187, umesitishwa hadi tarehe ya uchaguzi wa kwanza wa mabunge ya kaunti na magavana utakaofanywa chini ya Katiba hii.

(3)Licha ya ibara ndogo ya (2)—

(a)uchaguzi wa mabunge ya kaunti na magavana utafanywa kwa mujibu wa Vifungu vya 177 na 180 vya Katiba hii; na

(b)sheria zinazohusu serikali ya ugatuzi, zinazohitajiwa na Ambatisho hili na Sura za Kumi na Moja na Kumi Mbili za Katiba hii, zitatungwa katika muda uliowekwa chini ya Ambatisho la Tano.

(4)Kutekelezwa kwa Kifungu cha 62 (2) na (3) kutasitishwa hadi Tume ya Ardhi ya Kitaifa itakapobuniwa.

3. Kuongezwa kwa muda wa kutumia vifungu vya Katiba ya awali

(1)Hadi Bunge litakapopitisha Sheria inayotarajiwa katika Vifungu vya 15 na 18, sehemu ya 93 ya Katiba ya awali itaendelea kutumika.

(2)Sehemu za 30 hadi 40, 43 hadi 46, na 48 hadi 58 za Katiba ya awali, vifungu vya Katiba ya awali vinavyohusu kitengo cha serikali kinachosimamia utendaji na Sheria Kuhusu Muungano wa Kitaifa na Maridhiano zitaendelea kutumika hadi uchaguzi mkuu wa kwanza utakapofanywa chini ya Katiba hii, lakini vifungu vya Katiba hii kuhusu mfumo wa uchaguzi, ustahiki wa kuchaguliwa na mchakato wa uchaguzi vitatumika katika uchaguzi huo.

(3)Hadi Tume ya Huduma za Polisi za Kitaifa iliyotajwa katika Kifungu cha 246 itakapobuniwa, sehemu ya 108(2) ya Katiba ya awali itatumika katika uteuzi, hatua za kinidhamu na kuondolewa ofisini katika Huduma za Polisi za Kitaifa.

4. Kamati Teule ya Bunge

Kutakuwa na kamati teule ya Bunge la Kitaifa itakayojulikana kama Kamati ya Kusimamia Utekelezaji wa Katiba, itakayowajibika katika kusimamia utekelezaji wa Katiba hii, na ambayo, kati ya masuala mengine—

(a)itapokea ripoti za mara kwa mara kutoka kwa Tume ya Utekelezaji wa Katiba kuhusu utekelezaji wa Katiba hii, ikijumuisha ripoti kuhusu—

(i)maandalizi ya sheria yanayohitajiwa na Katiba hii na changamoto zozote kuhusu maandalizi hayo;

(ii)mchakato wa kubuni tume mpya;

(iii)mchakato wa kuunda miundombinu inayohitajika ili kutekeleza shughuli za kila kaunti kwa njia mwafaka ikijumuisha hatua zilizopigwa katika kuweka ofisi na mabunge pamoja na kuajiri na kuhamisha wafanyakazi.

(iv)ugatuzi wa mamlaka na majukumu kwa kaunti chini ya sheria inayobainishwa katika sehemu ya 15 ya Ambatisho hili; na

(v)vizuizi vyovyote katika mchakato wa kutekeleza Katiba hii;

(b)itashirikiana na Mwanasheria Mkuu, Tume ya Utekelezaji wa Katiba na kamati husika za Bunge ili kuhakikisha sheria zinazohitajiwa na Katiba hii zimewasilishwa bungeni na kupitishwa kwa wakati ufaao; na

(c)itachukua hatua zinazofaa kuhusiana na ripoti hizo ikijumuisha kutatua matatizo yoyote katika utekelezaji wa Katiba hii.

5. Tume ya Utekelezaji wa Katiba

(1)Tume ya Utekelezaji wa Katiba imebuniwa.

(2)Tume hiyo inajumuisha—

(a)mwenyekiti; na

(b)wanachama wengine nane.

(3)Wanachama wa Tume—

(a)watajumuisha watu wenye uzoefu katika masuala ya usimamizi wa umma, haki za binadamu na serikali; na

(b)haitajumuisha mtu yeyote aliyehudumu kama mwanachama katika Tume ya Wataalamu iliyoteuliwa chini ya Sheria ya Marekebisho ya Katiba ya Kenya, 2008.

(4)Vifungu vya 248 na 254 vinatumika kwa Tume hiyo.

(5)Baada ya Tume ya Ugavi wa Mapato kubuniwa, Tume ya Utekelezaji wa Katiba itatuma notisi ya mikutano yake kwa Tume hiyo, na mwanachama wa Tume ya Ugavi wa Mapato ataruhusiwa kuhudhuria na kushiriki katika mikutano yoyote kama hiyo, lakini hatapiga kura.

(6)Majukumu ya Tume hiyo yatakuwa ni—

(a)kufuatilia, kusimamia na kuwezesha utungaji wa sheria na taratibu za kiutawala zinazohitajika ili kutekeleza Katiba hii;

(b)kushirikiana na Mwanasheria Mkuu na Tume ya Marekebisho ya Sheria ya Kenya katika kutayarisha sheria itakayowasilishwa Bungeni ambayo itahitajika ili kutekeleza Katiba hii; na

(c)itatoa ripoti za mara kwa mara kwa Kamati ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Katiba. Kamati ya Usimamizi—

(i)hatua zilizopigwa katika utekelezaji wa Katiba hii; na

(ii)vizuizi vyovyote katika utekelezaji wake; na

(d)itafanya kazi na kila tume ya kikatiba kuhakikisha kuwa madhumuni na vifungu vya Katiba hii vinaheshimiwa.

(7)Tume ya Utekelezaji wa Katiba hii itavunjwa miaka mitano baada ya kubuniwa kwake au baada ya kutekelezwa kikamilifu kwa Katiba hii kama itakavyoamuliwa na Bunge, yoyote kati ya hatua hizi itakayotimia mwanzo ikichukuliwa, lakini Bunge la Kitaifa linaweza kuiongezea muda Tume hiyo kwa uamuzi.

Sehemu ya 2—Majukumu, Sheria na Haki Zilizopo

6. Haki, majukumu na Wajibu wa Serikali

Isipokuwa Katiba hii inapoeleza vinginevyo, haki na majukumu yote ya Serikali au Jamhuri, bila kujalisha yalivyotokea, na ambayo yalikuwepo kabla ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii yataendelea kama haki na majukumu ya serikali ya kitaifa au Jamhuri chini ya Katiba hii.

7. Sheria zilizopo

(1)Sheria zote zinazotumika kabla ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii zitaendelea kutumika na zitafasiriwa kwa kuzingatia mabadiliko yatakayoweza kuambatanishwa na Katiba hii. Ikiwa, kwa mujibu wa suala lolote—

(a)sheria iliyokuwa ikitumika kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii inatoa majukumu kwa kitengo fulani cha Serikali au afisa wa umma; na

(b)kifungu katika Katiba hii kinachotumika kinatoa majukumu kuhusu suala hilo kwa kitengo tofauti cha Serikali au afisa wa umma, vifungu vya Katiba hii vitatawala kwa kiwango cha ukinzani huo.

8. Ardhi iliyopo na makubaliano kuhusu mali-asili

(1)Katika tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii ardhi yoyote inayomilikiwa na mtu ambaye si raia wa Kenya itarejeshwa kwa Jamhuri ya Kenya ili kumilikiwa kwa niaba ya wananchi wa Kenya, na Serikali itampa mtu huyo kipindi cha miaka tisini na tisa cha kukodisha ardhi hiyo na kumtoza kiasi kidogo cha kodi.

(2)Katika tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii, umiliki au haki zozote katika ardhi ambazo zinazidi muda wa kukodisha ardhi kwa miaka tisini na tisa, ardhi hiyo ikimilikiwa na mtu ambaye sio raia, itabadilishwa na kuwa ardhi inayokodishwa kwa muda wa miaka tisini na tisa.

(3)Mwongozo unaotolewa na Kifungu cha 71 hautatekelezwa hadi sheria inayorejelewa katika Kifungu hicho itungwe.

Sehemu ya 3—Serikali ya Kitaifa

9. Uchaguzi na uchaguzi mdogo

(1)Uchaguzi wa kwanza wa Rais, Bunge la Kitaifa, Seneti, mabunge ya kaunti na magavana wa kaunti chini ya Katiba hii utafanywa kwa wakati mmoja, katika muda wa siku sitini baada ya kuvunjwa kwa Bunge la Kitaifa mwishoni mwa muhula wake.

(2)Licha ya ibara ndogo ya (1), ikiwa muungano uliobuniwa chini ya Maridhiano ya Kitaifa umevunjwa na uchaguzi mkuu kufanywa kabla ya mwaka wa 2012, uchaguzi wa kwanza wa mabunge ya kaunti na magavana utafanywa katika mwaka huo wa 2012.

10. Bunge la Kitaifa

Bunge la Kitaifa lililokuwa kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii litaendelea kama Bunge la Kitaifa kwa madhumuni ya Katiba hii kwa muhula wake uliosalia.

11. Seneti

(1)Hadi Seneti ya kwanza itakapochaguliwa chini ya Katiba hii—

(a)majukumu ya Seneti yatatekelezwa na Bunge la Kitaifa; na

(b)jukumu lolote au mamlaka yoyote yanayohitajika kutekelezwa kwa pamoja na vitengo vyote viwili vya Bunge au kitengo kimoja baada ya kingine, yatatekelezwa na Bunge la Kitaifa.

(2)Jukumu lolote au mamlaka ya Seneti, ikiwa yatatekelezwa na Bunge la Kitaifa kabla ya tarehe inayobainishwa katika ibara ndogo ya (1), yatachukuliwa kuwa yalitekelezwa kikamilifu na Seneti.

12. Kitengo cha Serikali Kinachosimamia Utendaji

(1)Watu wanaohudumu katika ofisi za Rais na Waziri Mkuu kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, wataendelea kuhudumu kama Rais na Waziri Mkuu mtawalia, kwa mujibu wa Katiba ya awali na Sheria Kuhusu Muungano na Maridhiano ya Kitaifa ya mwaka wa 2008 hadi uchaguzi mkuu ufanyike chini ya Katiba hii, isipokuwa waondoke ofisini kwa mujibu wa Katiba ya awali na Sheria hiyo ya Maridhiano.

(2)Watu wanaohudumu katika ofisi za Makamu wa Rais na Naibu Waziri Mkuu au wanahudumu katika Baraza la Mawaziri au kama Waziri Msaidizi kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, wataendelea kuhudumu kulingana na Katiba ya awali hadi uchaguzi mkuu wa kwanza utakapofanywa chini ya Katiba hii, isipokuwa waondoke au kuondolewa ofisini kulingana na Katiba ya awali na Sheria Kuhusu Muungano na Maridhiano ya mwaka wa 2008.

(3)Mtu aliyechaguliwa kuwa Rais kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii hastahiki kugombea uchaguzi wa urais chini ya Katiba hii.

13. Kiapo cha uaminifu kwa Katiba hii

Katika tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii, Rais na afisa yeyote wa Serikali, au mtu yeyote ambaye kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii alikuwa amekula kiapo au kutoa uthibitisho wa kuhudumu katika ofisi hiyo chini ya Katiba ya awali, au anayetakiwa kula kiapo au kutoa uthibitisho chini ya Katiba hii, ataapa au kutoa uthibitisho ufaao chini ya Katiba hii.

Sehemu ya 4—Serikali ya Ugatuzi

14. Kutumika kwa vifungu vinavyohusiana na Serikali ya ugatuzi

(1)Sheria zinazotajwa katika sehemu ya 2 (3) (b) na ya 15 zinaweza kupitishwa tu baada ya Tume ya Utekelezaji wa Katiba na, ikiwa Tume ya Ugavi wa Mapato imebuniwa, Tume hiyo pia imetoa mashauri na mapendekezo yoyote ya Tume hizo yamezingatiwa na Bunge.

(2)Tume hizo zitapewa angalau siku thelathini ili kutathmini sheria chini ya ibara ndogo ya (1).

(3)Ibara ndogo za (1) na (2) hazitatumika tena Tume ya Utekelezaji wa Katiba itakapovunjwa.

15. Mwongozo kuhusu ugatuzi wa majukumu kutolewa na Sheria ya Bunge

(1)Bunge, kupitia kwa sheria, litatoa mwongozo wa kuhamishwa kwa awamu, wa majukumu kutoka kwa serikali ya kitaifa hadi serikali za kaunti kama yalivyotolewa chini ya Kifungu cha 185, kwa kipindi kisichozidi miaka mitatu kuanzia tarehe ya uchaguzi wa kwanza wa mabunge ya kaunti.

(2)Sheria inayotajwa katika ibara ndogo ya (1)—

(a)itatoa mwongozo wa jinsi serikali ya kitaifa—

(i)itakavyowezesha ugatuzi wa mamlaka;

(ii)itakavyosaidia serikali za kaunti kujenga uwezo wao wa kujitawala na wa kutoa huduma zinazostahili kutolewa na serikali hizo; na Kiapo cha uaminifu kwa Katiba hii.

(iii)itatoa msaada kwa serikali za kaunti;

(b)itaweka vigezo ambavyo lazima vitimizwe kabla ya majukumu fulani kugatuliwa kwa serikali za kaunti, ili kuhakikisha kwamba serikali hizo hazipewi majukumu ambayo haziwezi kuyatekeleza; na

(c)itaruhusu ugatuzi wa mamlaka ili kuhakikisha kwamba majukumu yanagatuliwa kwa haraka kwa kaunti ambazo zina uwezo wa kuyatekeleza, lakini kwamba hakuna kaunti iliyopewa majukumu isiyoweza kutekeleza; na

(d)itatoa mikakati ambayo itahakikisha kwamba Tume ya Utekelezaji wa Katiba inaweza kutekeleza jukumu lake la kufuatilia utekelezaji wa mfumo wa serikali ya ugatuzi kwa ufanisi.

16. Ugavi wa mapato

Licha ya Kifungu cha 217 (1), maamuzi ya kwanza na ya pili kuhusu misingi ya ugavi wa mapato kati ya kaunti yatafanywa kila baada ya miaka mitatu, badala ya kila baada ya miaka mitano kama inavyoelezewa katika Kifungu hicho.

17. Utawala wa Mikoa

Katika kipindi cha miaka mitano baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, serikali ya kitaifa itafanya marekebisho katika mfumo wa utawala unaojulikana kama utawala wa mikoa, ili uafikiane na kuheshimu mfumo wa serikali ya ugatuzi uliobuniwa chini ya Katiba hii.

18. Ofisi za Utawala wa Mitaa

Ofisi zote za utawala wa ndani zilizobuniwa chini ya Sheria Kuhusu Serikali za Mitaa (Sura ya 265 ya Sheria za Kenya) zilizokuwa kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii zitaendelea kuwepo lakini kwa kuzingatia sheria yoyote inayoweza kupitishwa.

Sehemu ya 5 – Utekelezaji wa Haki

19. Kanuni za utekelezaji wa Sheria za Haki

Hadi Jaji Mkuu atakapotengeneza kanuni zinazorejelewa katika Kifungu cha 22, Kanuni za utekelezaji wa haki na uhuru wa kimsingi chini ya sehemu ya 84 (6) ya Katiba ya awali zitaendelea kutumika lakini kwa kuzingatia mabadiliko muhimu yatakayoziambatanisha na Kifungu cha 22.

20. Tume ya Huduma za Mahakama;

(1)Tume ya Huduma za Mahakama itateuliwa katika muda wa siku sitini baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, na Tume hiyo itachukuliwa kuwa imebuniwa ipasavyo chini ya Katiba hii licha ya kwamba huenda kukawa na nafasi wazi katika uanachama wake kwa kuwa idara zozote zinazowateua au kuwachagua wanachama hazijafanya hivyo.

(2)Licha ya ibara ndogo ya (1), Tume ya Huduma za Mahakama haitatekeleza majukumu yake isipokuwa wanachama watano wameteuliwa.

(3)Ili kuhakikisha kuwa kuna mwendelezo katika shughuli za Tume ya Huduma za Mahakama, licha ya Kifungu cha 171 (4), Tume itakapobuniwa kwa mara ya kwanza, wanachama wafuatao watateuliwa ili kuhudumu kwa miaka mitatu pekee—

(a)

(A)Jaji wa Mahakama ya Rufaa aliyeteuliwa chini ya Kifungu cha 171 (c);

(b)jaji wa Mahakama Kuu aliyeteuliwa chini ya Kifungu cha 171 (4) (d);

(c)mmoja kati ya wakili walioteuliwa chini ya Kifungu cha 171 (4) (f), watakaotambuliwa na shirika la kisheria linalowajibika katika udhibiti wa kitaalam wa mawakili; na

(d)mmoja wa wanachama walioteuliwa na Rais chini ya Kifungu cha 171 (4) (h); atakayetambuliwa na Rais.

(4)Hadi Tume ya Huduma za Umma inayorejelewa katika Kifungu cha 233 itakapobuniwa, mtu aliyeteuliwa na Tume ya Huduma za Umma chini ya sehemu ya 106 ya Katiba ya awali atahudumu katika Tume ya Huduma za Mahakama lakini, Tume mpya ya Huduma za Umma itakapobuniwa, mtu huyo atawacha kuwa mwanachama wa Tume ya Huduma za Mahakama na Tume hiyo mpya ya Huduma za Umma itamteua mtu atakayehudumu katika Tume ya Huduma za Mahakama.

21. Kuundwa kwa Mahakama ya Juu Zaidi

(1)Kubuniwa kwa Mahakama ya Juu Zaidi na kuteuliwa kwa majaji wa Mahakama hiyo kutakamilishwa katika muda wa mwaka mmoja kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

(2)Hadi Mahakama ya Juu Zaidi itakapobuniwa, Mahakama ya Rufaa itakuwa na mamlaka katika kesi zinazopaswa kusikizwa na kuamuliwa na Mahakama ya Juu Zaidi.

22. Usikilizaji wa kesi na kesi ambazo hazijakamilika

Kesi zote ambazo hazijakamilika katika mahakama yoyote zitaendelea kusikilizwa na uamuzi kutolewa na mahakama iliyokuwa ikisikiza kesi hiyo au mahakama ya kiwango sawa iliyobuniwa chini ya Katiba hii au itakavyoelekezwa na Jaji Mkuu au Msajili wa Mahakama Kuu.

23. Majaji

(1)Katika muda wa mwaka mmoja baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, Bunge litatunga sheria itakayotekelezwa licha ya Kifungu cha 160, 167 na 168, ambayo itaweka mikakati na utaratibu wa kukagua ustahiki wa majaji na mahakimu wote waliokuwa ofisini mnamo tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, wa kuendelea kuhudumu kwa mujibu wa maadili na kanuni zilizotolewa katika Vifungu vya 10 na 159, muda huo wa kukaguliwa ukiamuliwa katika sheria hiyo.

(2)Kuondolewa au utaratibu utakaopelekea kuondolewa kwa jaji kutoka ofisini kwenye msingi wa utekelezaji wa sheria inayorejelewa katika ibara ndogo ya (1) hakutapingwa au kukaguliwa na mahakama yoyote.

24. Jaji Mkuu

(1)Jaji Mkuu aliye ofisini kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, ataondoka ofisini katika muda wa miezi sita baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii na anaweza kuchagua—

(a)kustaafu kutoka katika kitengo cha mahakama; au

(b)kwa kuzingatia mchakato wa ukaguzi huo chini ya sehemu ya 23, kuendelea kuhudumu katika Mahakama ya Rufaa.

(2)Jaji Mkuu mpya atateuliwa na Rais, kwa kuzingatia Sheria Kuhusu Muungano wa Kitaifa na Maridhiano, na baada ya kushauriana na Waziri Mkuu na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa.

(3)Ibara ndogo ya (2) pia itatumika ikiwa kuna nafasi za ziada katika ofisi ya Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi mkuu wa kwanza chini ya Katiba hii.

Sehemu ya 6 – Tume na Ofisi

25. Tume za Kikatiba

(1)Tume ya Utekelezaji wa Katiba na Tume ya Ugavi wa Mapato zitabuniwa katika muda wa siku tisini baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

(2)Tume ya Mishahara na Malipo itabuniwa katika muda wa miezi tisa baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

(3)Hadi sheria inayorejelewa katika Kifungu cha 256 itakapoanza kutumika, watu watakaoteuliwa kama wanachama au mwenyekiti wa Tume ya Mishahara na Malipo watateuliwa na Rais, kwa kuzingatia Sheria Kuhusu Muungano wa Kitaifa na Maridhiano, na baada ya kushauriana na Waziri Mkuu na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa.

26. Tume ya Kitaifa Kuhusu Haki za Binadamu na Usawa ya Kenya

(1)Makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa ya Kenya walioteuliwa chini ya Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ya Kenya ya mwaka wa 2002 (Na. 9 ya 2002) na makamishna wa Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Maendeleo walioteuliwa chini ya Sheria ya Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Maendeleo ya mwaka wa 2003 (Na. 13 ya 2003), mbali na Makatibu Wakuu na Mwanasheria Mkuu au mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu, watakuwa wanachama wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa kwa muhula wao uliosalia, lakini kila mmoja wao atadumisha masharti yake ya utendakazi yalivyokuwa mnamo tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

(2)Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu ndiye atakayekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa kwa muhula uliosalia wa mwenyekiti huyo, na mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Jinsia na Maendeleo atakuwa Naibu Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa ya Kenya kwa muda wa muhula wa mwenyekiti huyo uliosalia.

27. Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi

(1)Tume ya Mipaka iliyobuniwa chini ya Katiba ya awali itaendelea kuhudumu kama ilivyobuniwa katika Katiba hiyo na kwa masharti ya sehemu za 41 B na 41 C lakini—

(a)haitaweka mipaka ya kaunti zilizobuniwa chini ya Katiba hii;

(b)itaweka mipaka ya maeneo bunge na wadi ikitumia vigezo vilivyotajwa katika Katiba hii; na

(c)wanachama wa Tume hiyo watakuwa chini ya Sura ya Saba ya Katiba hii.

(2)Hitaji katika Kifungu cha 89 (2) kwamba ukaguzi wa mipaka ya maeneo bunge na wadi utakamilishwa angalau miezi kumi na miwili kabla ya uchaguzi mkuu halitumiki katika ukaguzi wa mipaka kabla ya uchaguzi wa kwanza chini ya Katiba hii.

(3)Tume ya Mipaka itahakikisha kuwa ukaguzi wa kwanza wa mipaka ya maeneo bunge utakaofanywa chini ya Katiba hii hautasababisha kupotea kwa eneo bunge lililokuwepo katika tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

28. Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka

(1)Tume Huru ya Muda ya Uchaguzi iliyobuniwa chini ya sehemu ya 41 ya Katiba ya awali itaendelea kuhudumu ofisini kwa mujibu wa Katiba hiyo kwa muda wa muhula uliosalia au hadi Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itakayobuniwa chini ya Katiba hii ibuniwe, hali itakayotokea mwisho ikitumiwa.

(2)Wanachama wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka watakapoteuliwa, hitaji la kuendeleza na kudumisha ustadi na uzoefu utazingatiwa.

29. Uteuzi mpya

(1)Mchakato wa uteuzi wa watu ili kujaza nafasi zitakazotokea kutokana na kutekelezwa kwa Katiba hii, utaanza mnamo tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii na kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.

(2)Isipokuwa Ambatisho hili litoe mwongozo vinginevyo, Katiba hii inapohitaji uteuzi ufanywe na Rais na kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, hadi baada ya uchaguzi wa kwanza chini ya Katiba hii, kwa kuzingatia Sheria Kuhusu Muungano wa Kitaifa na Maridhiano, Rais atamteua mtu baada ya kushauriana na Waziri Mkuu na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa.

Sehemu ya 6—Masuala ya Ziada

30. Uraia kwa kuzaliwa

Raia wa Kenya ni raia kwa kuzaliwa ikiwa raia huyo—

(1)alipata uraia chini ya Kifungu cha 87 au 88 (1) cha Katiba ya awali; au

(2)angepata uraia ikiwa Kifungu cha 87 (2) kingesema ifuatavyo:

“ Kila mtu ambaye alizaliwa nje ya Kenya, na mnamo tarehe 11 Desemba, 1963 ni raia wa Uingereza na Koloni zake au mtu aliyepata ulinzi wa Uingereza, mtu huyo atakuwa, iwapo mama au baba yake atakuwa, au isipokuwa kufariki kwake angekuwa raia wa Kenya kwa mujibu wa ibara ndogo ya (1), atakuwa raia wa Kenya mnamo tarehe 12 Desemba, 1963.”

31. Ofisi zilizopo

(1)Isipokuwa Ambatisho hili litoe mwongozo vinginevyo, mtu ambaye kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii alikuwa anahudumu au kutoa huduma kwa muda katika ofisi iliyobuniwa na Katiba ya awali, kufikia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii ataendelea kuhudumu au kutoa huduma kwa muda katika ofisi hiyo chini ya Katiba hii kwa muda uliosalia wa muhula wa mtu huyo, iwapo kuna muda wowote uliosalia.

(2)Kwa kuzingatia ibara ndogo ya (7) na sehemu ya 24, mtu ambaye kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii alikuwa anahudumu au kutoa huduma kwa muda katika ofisi ya umma iliyobuniwa kisheria, ataendelea kuhudumu au kutoa huduma kwa muda katika ofisi hiyo kwa kiwango kinachoambatana na Katiba hii, kana kwamba aliteuliwa kwa nafasi hiyo chini ya Katiba hii.

(3)Vifungu vya sehemu hii havitaathiri mamlaka yaliyotolewa kwa mtu yeyote au shirika chini ya Katiba hii au sheria ya kuvunja ofisi au kuwaondoa watu kutoka ofisi inayorejelewa katika ibara ndogo ya (2).

(4)Ikiwa mtu ameondoka katika ofisi ambayo alikuwa akihudumu kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, na ofisi hiyo ipo au imeundwa chini ya Katiba hii, ikiwa atastahiki, anaweza kuteuliwa, kuchaguliwa tena, au vinginevyo kuteuliwa ili kuhudumu katika ofisi hiyo kulingana na vifungu vya Katiba hii, isipokuwa kwa kiwango ambacho Katiba hii inatoa mwongozo vinginevyo.

(5)Majukumu ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma yatatekelezwa na Mwanasheria Mkuu hadi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atakapoteuliwa chini ya Katiba hii.

(6)Majukumu ya Msimamizi wa Bajeti yatatekelezwa na Mkaguzi Mkuu hadi Msimamizi wa Bajeti atakapoteuliwa chini ya Katiba hii.

(7)Licha ya ibara ndogo ya (1), Mwanasheria Mkuu na Mkaguzi Mkuu wataendelea kuhudumu ofisini kwa kipindi kisichopungua miezi kumi na miwili baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, na uteuzi utakaofuata katika ofisi hizi utakuwa chini ya Katiba hii.

32. Malipo ya uzeeni, bahashishi na manufaa mengine

Sheria inayotumika katika malipo ya uzeeni kwa maafisa wa ofisi za kikatiba chini ya Katiba ya awali itakuwa sheria iliyotumika wakati manufaa hayo yalipotolewa au sheria yoyote itakayokuwa ikitumika hapo baadaye na ambayo haitamwathiri vibaya mtu huyo.

33. Taasisi, ofisi, mali na madeni kurithiwa

Ofisi au taasisi ambayo ilibuniwa chini ya Katiba hii ndio inayorithi kisheria, ofisi au taasisi iliyokuwepo, ambayo ilibuniwa chini ya Katiba ya awali au Sheria ya Bunge iliyokuwa ikitumika kabla ya tarehe ya kutumika kwa Katiba hii, ofisi au taasisi hiyo iwe inajulikana kwa jina lile lile au jina jipya.

34. Sarafu

Hakuna chochote katika Kifungu cha 231 (4) kinachoathiri uhalali wa sarafu na noti zilizotolewa kabla ya tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba hii.

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho