Uchaguzi wa wabunge
(1)Uchaguzi mkuu wa wabunge katika Bunge la Kitaifa na katika Seneti utafanyika katika Jumanne ya pili ya mwezi wa Agosti katika kila mwaka wa tano.
(2)Panapotokea nafasi katika ofisi ya mbunge katika Bunge la Kitaifa chini ya Kifungu cha 97 (1) (c), au katika Seneti chini ya Kifungu cha 98 (1) (b), (c) au (d), Spika anayehusika atatoa notisi ya nafasi hiyo kwa njia ya maandishi ndani ya siku ishirini na moja za kutokea kwa nafasi hiyo, na notisi hiyo itatolewa kwa maandishi kuhusu nafasi hiyo ya kazi kwa—
(a)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka; na
(b)chama cha kisiasa ambacho kupitia kwa orodha ya chama hicho, mwanachama huyo alichaguliwa au kuteuliwa.
(3)Nafasi hiyo iliyotajwa katika ibara ya (2), kwa kuzingatia ibara ya (5), itajazwa kwa namna iliyoagizwa na Sheria ya Bunge ndani ya siku ishirini na moja baada ya Spika anayehusika kuarifu kuhusu nafasi hiyo.
(4)Panapotokea nafasi ya kazi katika ofisi ya mwanachama wa Bunge la Kitaifa aliyechaguliwa chini ya Kifungu cha 97 (1) (a) au (b), au wa Seneti aliyechaguliwa chini ya Kifungu cha 98 (1) (a)—
(a)Spika anayehusika, katika muda wa siku ishirini na moja baada ya kutokea kwa nafasi hiyo, atatoa notisi kwa njia ya maandishi kuhusu nafasi hiyo kwa kuiandikia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka; na
(b)uchaguzi mdogo utafanyika katika muda wa siku tisini baada ya kutokea kwa nafasi hiyo, lakini kwa kuzingatia ibara ya (5).
(5)Nafasi iliyotajwa katika ibara ya (4) haitajazwa katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.