Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nane · Mabunge

Kifungu cha 115

Kif.115

Idhini na rufaa ya rais

(1)Katika siku kumi na nne baada ya kupokea Mswada, Rais—

(a)atauidhinisha Mswada huo; au

(b)ataurejesha Mswada Bungeni ili kujadiliwa upya na Bunge huku likizingatia sababu zozote alizonazo Rais kuhusu mswada huo.

(2)Ikiwa Rais ataurejesha Mswada bungeni ili ujadiliwe tena, Bunge, kwa kuzingatia taratibu zinazofaa chini ya Sehemu hii, linaweza—

(a)kuurekebisha Mswada huo kwa kuzingatia sababu alizotoa Rais; au

(b)kuupitisha Mswada huo kwa mara ya pili bila kufanya marekebisho.

(3)Ikiwa Bunge litarekebisha Mswada huo na kuzingatia mapendekezo ya Rais kikamilifu, Spika anayehusika atauwasilisha tena Mswada huo kwa Rais ili auidhinishe.

(4)baada ya kuzingatia sababu za Rais, linaweza kuupitisha Mswada huo kwa mara ya pili bila marekebisho au na marekebisho ambayo hayazingatii kikamilifu hoja zilizotolewa na Rais, kwa kura ambayo itaungwa mkono na—

(a)thuluthi mbili ya wabunge katika Bunge la Kitaifa; na

(b)thuluthi mbili ya wawakilishi katika Seneti, ikiwa ni Mswada unaohitaji idhini ya Seneti.

(5)Ikiwa Bunge litapitisha Mswada chini ya ibara ya (4)—

(a)Spika wa Bunge husika atawasilisha tena Mswada huo kwa Rais katika siku saba; na

(b)Rais atauidhinisha Mswada huo ndani ya siku saba.

(6)Ikiwa Rais hatauidhinisha Mswada huo au kuurejesha kwa wakati unaopendekezwa katika Ibara ya (1), au kuuidhinisha chini ya ibara ya (5) (b), Mswada huo utachukuliwa kuwa umeidhinishwa ifikiapo mwisho wa kipindi hicho.

Isome ndani ya Sura ya Nane →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho