Maamuzi ya Seneti
(1)Katika uchaguzi, wanachama wote wa Seneti ambao walikuwa wamesajiliwa kama wapiga kura katika kaunti fulani kwa pamoja watachukuliwa kama mjumbe mmoja kwa madhumuni ya ibara ya (4) na mwanachama aliyechaguliwa chini ya Kifungu cha (98) (1)(a) atakuwa kiongozi wa wajumbe hao.
(2)Seneti itakapopiga kura kuhusu suala lolote isipokuwa Mswada, Spika ataamua iwapo suala hilo linaathiri au haliathiri kaunti.
(3)Seneti inapopiga kura kuhusu suala ambalo haliathiri kaunti, kila seneta atakuwa na kura moja.
(4)Isipokuwa mwongozo utolewe vinginevyo katika Katiba hii, kwa suala lolote katika Seneti linalohusu kaunti—
(a)kila wajumbe wa kaunti watakuwa na kura moja itakayopigwa na kiongozi wa wajumbe hao kwa niaba ya, na endapo kiongozi wa wajumbe hao hayuko, kura itapigwa na mjumbe mwingine mmoja kati ya wajumbe hao ambaye ameteuliwa na kiongozi wa wajumbe hao;
(b)mtu ambaye atapiga kura kwa niaba ya wajumbe hao ataamua ikiwa atapiga kura kwa kuunga mkono au kutounga mkono suala hilo, baada ya kushauriana na wajumbe; au
(c)suala litakuwa limepitishwa ikiwa tu litaungwa mkono na wajumbe walio wengi.