Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tisa · Kitengo cha Serikali cha Utendaji

Kifungu cha 138

Kif.138

Mchakato wa uchaguzi wa rais

(1)Ikiwa ni mgombea mmoja wa urais atakayeteuliwa, mgombeaji huyo atatangazwa kuwa amechaguliwa.

(2)Ikiwa ni wagombeaji wawili wa urais watakaoteuliwa, uchaguzi utafanyika katika kila eneobunge.

(3)Katika uchaguzi wa rais—

(a)watu wote waliosajiliwa kama wapiga kura kwa madhumuni ya uchaguzi wa wabunge wana haki ya kupiga kura;

(b)uchaguzi utakuwa kwa njia ya siri katika siku ambayo imeelezewa chini ya ibara ya 101 (1) na kwa wakati, mahali na kwa njia ambayo imeagizwa chini ya Sheria ya Bunge; na

(c)baada ya kuhesabiwa kwa kura katika vituo vya kupigia kura, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itahesabu na kuhakikisha hesabu ya kura na kutangaza matokeo.

(4)Mgombea wa urais atatangazwa kuchaguliwa kama Rais ikiwa mgombea huyo atapokea—

(a)zaidi ya nusu ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi huo; na

(b)angalau asilimia ishirini na tano ya kura zilizopigwa katika kila kaunti, katika zaidi ya idadi nusu ya kaunti zote.

(5)Ikiwa hakuna mgombea atakayechaguliwa, uchaguzi mwingine utafanyika upya katika kipindi cha siku thelathini baada ya uchaguzi uliopita, na katika uchaguzi huo mpya, wagombeaji watakuwa tu—

(a)mgombea au wagombea ambao walipokea kura nyingi zaidi; na

(b)mgombeaji au wagombeaji ambao walipata idadi kubwa ya pili ya idadi ya kura.

(6)ikiwa wagombea zaidi ya mmoja atapokea idadi kubwa zaidi ya kura, ibara ya (5) (b) haitatumika na wagombeaji watakaokuwa katika uchaguzi mpya watakuwa wale ambao wamebainishwa katika ibara ya (5) (a).

(7)mgombeaji atakayepokea idadi kubwa zaidi ya kura katika uchaguzi mpya ndiye atakayetangazwa kuwa Rais.

(8)uchaguzi wa urais utafutiliwa mbali na uchaguzi mwingine mpya kufanyika ikiwa—

(a)hakuna mtu ambaye ameteuliwa kama mgombea kabla ya kumalizika kwa kipindi kilichowekwa cha kuwasilisha walioteuliwa;

(b)mgombeaji wa uchaguzi wa Rais au wa Naibu wa Rais atafariki katika au kabla ya tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi; au

(c)mgombea uchaguzi ambaye alistahili kutangazwa kuwa amechaguliwa kama Rais, atafariki kabla ya kutangazwa kuwa amechaguliwa kama Rais.

(9)Uchaguzi mpya wa urais chini ya ibara ya (8) utafanyika katika muda wa siku sitini baada ya tarehe iliyokuwa imewekwa ya uchaguzi uliopita.

(10)Katika muda wa siku saba baada uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka—

(a)atangaza matokeo ya uchaguzi; na

(b)atawasilisha taarifa iliyoandikwa ya matokeo ya uchaguzi kwa Jaji Mkuu na Rais aliye mamlakani.

Kwenye kura yako ya 2027

Kifungu hiki kinahusu chaguzi hizi

Isome ndani ya Sura ya Tisa →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho