Kuchaguliwa na Kuapishwa kwa Naibu wa Rais
(1)Kila mgombea katika uchaguzi wa urais atateua mtu ambaye anastahiki kuteuliwa kuwa mgombeaji wa urais, kama mgombeaji wa kiti cha Naibu wa Rais.
(2)Kwa madhumuni ya ibara ya (1), hakutakuwa na mchakato tofauti wa kumteua Naibu wa Rais na Kifungu cha 137 (1) (d) hakitatumika kwa mgombea wa kiti cha Naibu wa Rais.
(3)Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka itamtangaza mgombeaji aliyeteuliwa na mtu ambaye amechaguliwa kuwa Rais, kuwa amechaguliwa kama Naibu wa Rais.
(4)Kuapishwa kwa Naibu wa Rais mteule kutafanyika mbele ya Jaji Mkuu, au iwapo Jaji Mkuu hayupo, mbele ya Naibu wa Jaji Mkuu na kwa uwazi.
(5)Naibu wa Rais mteule atachukua hatamu za uongozi kwa—
(a)kula kiapo au kutoa uthibitisho wa uaminifu; na
(b)Kula kiapo au kutoa uthibitisho wa kutekeleza majukumu ya ofisi,kama ilivyoagizwa katika Ambatisho la Tatu.
(6)Muhula wa kuhudumu kama Naibu wa Rais utaanzia tarehe ya kuapishwa kwa Naibu wa Rais, na utakamilika—
(a)wakati ambapo mtu atakayechaguliwa kuwa Rais anayefuata katika uchaguzi chini ya Kifungu cha (136) (2) (a) ataapishwa;
(b)Naibu wa Rais anapohudumu kama Rais; au
(c)kwa kijiuzulu, kufariki au kuondolewa mamlakani kwa Naibu wa Rais.
(7)Naibu wa Rais anaweza, kwa wakati wowote, kujiuzulu kwa kumwandikia barua Rais na kujiuzulu huko kutatekelezeka katika saa na tarehe iliyobainiwa katika barua hiyo, au ikiwa tarehe haijabainishwa, adhuhuri ya siku ifuatayo baada ya kupokelewa kwa barua hiyo.
(8)Hakuna mtu yoyote atakayehudumu kama Naibu wa Rais kwa zaidi ya mihula miwili.