Baraza la Mawaziri
(1)Baraza la Mawaziri linajumuisha—
(a)Rais;
(b)Naibu wa Rais;
(c)Mwanasheria Mkuu; na
(d)Mawaziri wasiopungua kumi na wanne au wasiozidi ishirini na wawili.
(2)Rais atawapendekeza, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa kuwateua Mawaziri.
(3)Waziri hatakuwa Mbunge.
(4)Kila mtu atakayeteuliwa kama Waziri—
(a)ataanza kuhudumu kwa kuapa au kutoa thibitisho la uaminifu kwa watu na Jamhuri ya Kenya na kuapa kuitii Katiba hii, mbele ya Rais na kwa mujibu wa Ambatisho la Nne; na
(b)anaweza kujiuzulu kwa kumwasilishia Rais taarifa iliyoandikwa ya kujiuzulu kwake.
(5)Rais––
(a)anaweza kubadilisha wizara ambayo Waziri atahudumu;
(b)anaweza kumwachisha kazi Waziri; na
(c)atamwachisha kazi Waziri iwapo atahitajika kufanya hivyo, kwa uamuzi uliokubaliwa chini ya ibara ya (6) hadi (10).
(6)Mwanachama wa Bunge la Kitaifa anayeungwa mkono na angalau robo moja ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, anaweza kupendekeza hoja wa kumtaka Rais amwachishe kazi Waziri—
(a)kwenye msingi wa ukiukaji mkubwa wa Kifungu cha Katiba hii au sheria nyingine yoyote;
(b)Iwapo kuna sababu kuu za kuamini kwamba Waziri huyo amefanya uhalifu chini ya sheria ya kitaifa au ya kimataifa; au
(c)kwa msingi wa mwenendo mbaya zaidi ofisini.
(7)Ikiwa hoja chini ya ibara ya (5) itaungwa mkono na angalau thuluthi moja ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa—
(a)Bunge la Kitaifa litateua kamati maalum akayojumuisha wanachama kumi na mmoja kuchunguza suala hili; na
(b)katika muda wa siku kumi, kamati hii maalum itaripoti kwa Bunge la Kitaifa ikiwa limepata madai dhidi ya Waziri kuthibitishwa.
(8)Waziri ana haki ya kufika au kuwakilishwa mbele ya kamati maalum wakati wa uchunguzi wake.
(9)Ikiwa kamati hiyo maalum itaripoti kwamba imepata madai hayo
(a)othibitishwa, hakuna taratibu zingine zitakazofuatwa; au
(b)kuthibitishwa, Bunge la Kitaifa––
(i)litampa Waziri nafasi ya kusikizwa; na
(ii)litapiga kura ili kuidhinisha uamuzi unaomtaka Waziri kuachishwa kazi.
(10)Ikiwa uamuzi ulio chini ya ibara ya (8) unaomtaka Rais kumwachisha kazi Waziri utaungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge katika Bunge la Kitaifa––
(a)Spika atamwasilishia Rais uamuzi huu kwa haraka; na
(b)Rais atamwachisha kazi Waziri huyo.