Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tisa · Kitengo cha Serikali cha Utendaji

Kifungu cha 157

Kif.157

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma

(1)Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma imebuniwa.

(2)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atapendekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, atateuliwa na Rais.

(3)Ustahiki wa kuteuliwa kama Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ni sawa na zile wa uteuzi wa Jaji wa Mahakama Kuu.

(4)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atakuwa na mamlaka ya kumwagiza Inspekta Jenerali wa Huduma ya Polisi ya Kitaifa kuchunguza habari yoyote au madai ya vitendo vya jinai, na Inspekta Jenerali huyo atafuata maelekezo hayo.

(5)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atahudumu kwa muhula wa miaka minane na hatastahiki kuteuliwa tena.

(6)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atatekeleza mamlaka ya Serikali ya kufungua mashtaka na anaweza—

(a)kufungua mashtaka katika kesi ya uhalifu dhidi ya mtu yeyote katika mahakama yoyote (isipokuwa mahakama ya kijeshi) kutokana na kosa lolote linalodaiwa kufanywa;

(b)kuchukua na kuendeleza kesi zozote ya uhalifu zilizoanzishwa katika mahakama yoyote (isipokuwa katika mahakama ya kijeshi) na ambazo zilifunguliwa au kusimamiwa na mtu mwingine au mamlaka nyingine; na

(c)kwa mujibu wa ibara ya (7) na (8), kusitisha, kwa wakati wowote kabla ya hukumu kutolewa, kuendelea kwa kesi zozote za jinai, zilizowasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma au kuendelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya umma chini ya aya ya (b)

(7)Ikiwa kusitishwa kwa kesi zozote chini ya ibara ya (6) (c) kutafanyika baada ya upande wa mashtaka kufunga kesi yao, mshtakiwa ataachiliwa huru.

(8)Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ya Umma hawezi kusitisha kuendelea kwa kesi bila ruhusa ya mahakama.

(9)Mamlaka ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma yanaweza kutekelezwa naye kibinafsi au kupitia kwa maafisa wasaidizi watakaotekeleza mamlaka hayo kulingana na masharti maalum au ya kijumla.

(10)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma hatahitaji idhini ya mtu au mamlaka yoyote ili kuwasilisha kesi za kijinai, na katika kutekeleza mamlaka au majukumu yake hataelekezwa au kudhibitiwa na mtu au mamlaka yoyote.

(11)Katika kutekeleza mamlaka yaliyotolewa na Kifungu hiki, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atazingatia maslahi ya umma, utekelezaji wa haki na hitaji la kuzuia na kuepuka matumizi mabaya ya mchakato wa kisheria.

(12)Bunge linaweza kutunga sheria itakayotoa mamlaka ya kufungua mashtaka kwa taasisi zingine kando na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

Isome ndani ya Sura ya Tisa →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho