Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tisa · Kitengo cha Serikali cha Utendaji

Kifungu cha 158

Kif.158

Kuondolewa na kujiuzulu kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma

(1)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kuondolewa ofisini kwenye misingi ya—

(a)kutoweza kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo kutokana na kukosa uwezo wa kiakili au wa kimwili;

(b)kutozingatia Sura ya Sita;

(c)kufilisika;

(d)kutokuwa na uzoefu unaohitajika; au

(e)mwenendo mbaya zaidi ofisini au tabia mbaya.

(2)Mtu anayetaka kuondolewa mamlakani kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kuwasilisha ombi au malalamishi kwa Tume ya Huduma za Umma ambayo yatakuwa kwa njia ya maandishi, yakiainisha madai yanayounda msingi wa kuondolewa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma.

(3)Tume ya Huduma za Umma itajadili malalamishi hayo na ikiridhika kwamba yanafichua kuwepo kwa msingi wa kuondolewa ofisini chini ya Ibara ya (1), itawasilisha ombi au malalamishi hayo kwa Rais.

(4)Baada ya kupokea na kuchunguza ombi au malalamishi hayo, Rais, katika muda wa siku kumi na nne, atamsimamisha kazi Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kabla ya hatua kuchukuliwa na Rais kulingana na ibara ya (5) na kwa ushauri wa Tume ya Huduma za Umma, atateua kikundi cha watu watakaosikiza na kutoa uamuzi kuhusu ombi hilo, itakayojumuisha—

(a)wanachama wanne kutoka miongoni mwa wale ambao wanahudumu au wamewahi kuhudumu kama majaji katika mahakama ya ngazi ya juu, au wanaostahiki kuteuliwa kuwa majaji katika mahakama ya ngazi ya juu;

(b)wakili mmoja ambaye amehudumu kwa angalau miaka kumi na mitano na atakayeteuliwa na taasisi ya kisheria inayowajibika katika udhibiti wa taaluma ya mawakili; na

(c)watu wengine wawili walio na uzoefu katika masuala ya umma.

(5)Kikundi hicho kitachunguza swala hilo kwa haraka na kuripoti kuhusu ukweli uliopo na kutoa mapendekezo kwa Rais, ambaye atachukua hatua kulingana na mapendekezo ya kikundi hicho.

(6)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, ambaye amesimamishwa kazini kulingana na ibara ya (4) atapokea nusu ya mshahara wake hadi atakapoondolewa au kurudishwa ofisini kwake.

(7)Kikundi kitakachoteuliwa chini ya ibara ya (4) kitamchagua mwenyekiti miongoni mwao wanachama wake.

(8)Kikundi kitakachoteuliwa chini ya ibara ya (4) kitakuwa na jukumu la kudhibiti taratibu zake.

(9)Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma anaweza kujiuzulu kwa kumwandikia Rais notisi.

Isome ndani ya Sura ya Tisa →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho