Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi · Kitengo cha Serikali Kinachosimamia Mahakama

Kifungu cha 165

Kif.165

Mahakama Kuu

(1)Mahakama Kuu imebuniwa, ambayo—

(a)itakuwa na idadi ya majaji kama itakavyobainishwa katika Sheria ya Bunge;

(b)itapangwa na kusimamiwa kulingana na Sheria ya Bunge.

(2)Kutakuwa na Jaji Kinara wa Mahakama Kuu, ambaye atachaguliwa na majaji wa Mahakama Kuu kutoka miongoni mwao.

(3)Kwa kuzingatia ibara ya (5), Mahakama Kuu—

(a)Itakuwa na mamlaka ya kiasili katika kesi za jinai na kesi za kiraia;

(b)mamlaka ya kubaini iwapo haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki imezuiwa, kukiukwa, kuvunjwa au kutishiwa; au

(c)mamlaka ya kusikiliza kesi ya rufaa kutoka katika uamuzi wa taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama iliyoteuliwa chini ya Katiba hii kuchunguza kuondolewa kwa mtu ofisini, isipokuwa taasisi iliyoteuliwa chini ya Kifungu cha 144;

(d)mamlaka ya kusikiliza suala lolote kuhusu kufasiriwa kwa Katiba hii ikijumuisha—

(i)iwapo sheria yoyote haiambatani na, au inakiuka, Katiba hii;

(ii)iwapo chochote kinachosemekana kutekelezwa chini ya mamlaka ya Katiba hii au sheria yoyote, hakiambatani, au kinakiuka, Katiba hii;

(iii)suala lolote linalohusu mamlaka ya kikatiba ya vitengo vya serikali katika serikali za kaunti na suala lolote linalohusu uhusiano wa kikatiba kati ya ngazi za serikali; na

(iv)swali linalohusu mkinzano wa sheria chini ya Kifungu cha 191; na

(e)swala kuhusu mamlaka yake mengine yoyote, ya kiasili au ya rufaa, ambayo yametolewa na sheria.

(4)Suala lolote linalothibitishwa na mahakama kuwa linazua utata mkubwa kisheria chini ya ibara ya (3) (b) au (d) litasikilizwa na idadi isiyo shufwa ya majaji, na isiyopungua watatu, watakaoteuliwa na Jaji Mkuu.

(5)Mahakama Kuu haitakuwa na mamlaka kuhusiana na masuala—

(a)yaliyotengewa mamlaka ya kipekee ya Mahakama ya Juu Zaidi chini ya Katiba hii; au

(b)yaliyo chini ya mamlaka ya mahakama zilizotajwa katika Kifungu cha 162 (2).

(6)Mahakama Kuu ina mamlaka ya kusimamia mahakama za ngazi ya chini, mtu yeyote, taasisi au halmashauri inayotekeleza jukumu la kimahakama, lakini sio mahakama ya ngazi ya juu.

(7)Kwa malengo ya ibara ya (6), Mahakama Kuu inaweza kuitisha kumbukumbu za kesi yoyote inayoendelea katika mahakama ya ngazi ya chini, mtu, taasisi au halmashauri inayorejelewa katika ibara ya (6) na inaweza kutoa maagizo yoyote na kutoa maelekezo yanayofaa kwa maoni ya mahakama hiyo ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

Isome ndani ya Sura ya Kumi →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho