Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi · Kitengo cha Serikali Kinachosimamia Mahakama

Kifungu cha 166

Kif.166

Uteuzi wa Jaji Mkuu, Naibu wa Jaji Mkuu na majaji wengine

(1)Rais atateua—

(a)Jaji Mkuu na Naibu Jaji Mkuu kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma za Mahakama na kwa idhini ya Bunge; na

(b)majaji wengine wote, kulingana na mapendekezo ya Tume ya Huduma za Mahakama.

(2)Kila jaji wa mahakama ya ngazi ya juu atateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao—

(a)wana shahada ya sheria kutoka chuo kikuu kinachotambulika, au ni mawakili wa Mahakama Kuu, au wamehitimu kwa njia hii kutoka nchi nyingine inayotumia mfumo wa sheria unaokuzwa na majaji kupitia maamuzi yao;

(b)wana uzoefu unaohitajika chini ya ibara ya (3) hadi (6), bila kujalisha kwamba uzoefu huo ulipatikana nchini Kenya au katika nchi nyingine inayotumia mfumo wa sheria katika Jumuiya ya Madola; na

(c)wana mienendo na maadili mema, uadilifu na wasioegemea upande wowote.

(3)Jaji Mkuu na majaji wengine wa Mahakama ya Juu Zaidi watateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao—

(a)wana uzoefu wa angalau miaka kumi na mitano kama jaji katika mahakama ya ngazi ya juu; au

(b)wana uzoefu wa angalau miaka kumi na mitano kama wasomi wanaoheshimika, maafisa wa mahakama, wanasheria au uzoefu wa kiasi sawa katika nyanja nyingine ya kisheria inayohusika; au

(c)amehitimu kwa viwango vilivyotajwa katika aya ya (a) na (b) kwa muda wa miaka kumi na mitano kijumla;

(4)Kila jaji wa Mahakama ya Rufaa atateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao—

(a)wana uzoefu wa angalau miaka kumi kama jaji wa mahakama ya ngazi ya juu; au

(b)wana uzoefu wa angalau miaka kumi kama wasomi wanaoheshimika au wanasheria au uzoefu sawa katika nyanja nyingine ya kisheria inayohusika; au

(c)wamehitimu kulingana na aya ya (a) na (b) na kwa muda wa miaka kumi kijumla.

(5)Kila jaji wa Mahakama Kuu atateuliwa kutoka miongoni mwa watu ambao—

(a)wana uzoefu wa angalau miaka kumi kama jaji wa mahakama ya ngazi ya juu; au

(b)wana uzoefu wa angalau miaka kumi kama wasomi wanaoheshimika au wanasheria au uzoefu sawa katika nyanja nyingine ya kisheria inayohusika; au

(c)wamehitimu kwa viwango vilivyotajwa katika aya ya (a) na (b) na kwa muda wa miaka kumi kijumla.

Isome ndani ya Sura ya Kumi →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho