Uanachama katika bunge la kaunti
(1)(1) Bunge la kaunti linajumuisha—
(a)wanachama waliochaguliwa na wapiga kura waliosajiliwa katika wadi, uchaguzi huo ukifanyika siku ile ile ya uchaguzi mkuu wa wabunge, ambayo ni Jumanne ya pili ya mwezi Agosti baada ya kila miaka mitano na kila wadi ikijumuisha eneo la kuwakilishwa na mwanachama mmoja;
(b)idadi ya wabunge maalum inayohitajika ili kuhakikisha kwamba hakuna zaidi ya wabunge thuluthi mbili wa jinsia moja katika bunge hilo;
(c)idadi ya wanachama kutoka vikundi vya watu waliotengwa, wakiwemo watu wenye ulemavu na vijana, kama inavyoagizwa katika Sheria ya Bunge; na
(d)Spika, ambaye ni mwanachama aliyechaguliwa na wabunge.
(2)Wanachama wanaobainishwa katika ibara ya (1) (b) na (c) watateuliwa na vyama vya kisiasa kulingana na idadi ya viti ambavyo kila chama cha kisiasa kilipata katika uchaguzi wa kaunti hiyo chini ya ibara ya (a) kulingana na Kifungu cha 90.
(3)Kujazwa kwa viti maalum chini ya ibara ya (1) (b) kutaamuliwa baada ya kutangazwa kwa wanachama waliochaguliwa katika kila wadi.
(4)Bunge la kaunti linachaguliwa kwa muhula wa miaka mitano.