Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Moja · Serikali ya Ugatuzi

Kifungu cha 190

Kif.190

Usaidizi kwa serikali za kaunti

(1)Bunge litatunga sheria ili kuhakikisha kwamba serikali za kaunti zina usaidizi wa kutosha ili kuziwezesha kutekeleza majukumu yao.

(2)Serikali za kaunti zitaendesha mifumo ya usimamizi wa fedha inayoafikiana na matakwa ya sheria ya kitaifa.

(3)Bunge litatunga sheria itakayoruhusu serikali ya kitaifa kuingilia kati ikiwa serikali ya kaunti—

(a)imeshindwa kutekeleza majukumu yake; au

(b)haiendeshi mfumo wa usimamizi wa fedha unaoambatana na matakwa ya sheria ya kitaifa.

(4)Sheria inayorejelewa katika ibara ya (3) inaweza, hasa, kuipa serikali ya kitaifa mamlaka ya-—

(a)kuchukua hatua mwafaka ili kuhakikisha kwamba majukumu ya serikali ya kaunti yanatekelezwa na kwamba serikali hiyo inaendesha mfumo wa usimamizi wa fedha unaoafikia mahitaji yaliyotolewa; na

(b)kuwajibika katika utekelezaji wa majukumu husika ikiwa itahitajika.

(5)Sheria inayorejelewa chini ya ibara ya (3)—

(a)itahitaji notisi kutolewa kwa serikali ya kaunti kuhusu hatua zozote ambazo serikali ya kitaifa inanuia kuchukua;

(b)itaruhusu serikali ya kitaifa kuchukua tu hatua ambazo ni muhimu;

(c)itahitaji serikali ya kitaifa kuchukua hatua ambazo zitaisaidia serikali ya kaunti kurejelea kikamilifu utekelezaji wa majukumu yake serikali hiyo inapoingilia kati; na

(d)itatoa mchakato ambao Seneti inaweza kutumia ili kukomesha uingiliaji kati wa serikali ya kitaifa.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Moja →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho