Mgongano wa sheria
(1)Kifungu hiki kinahusu mgongano kati ya sheria za kitaifa na zile za kaunti, katika masuala ambayo viwango vyote viwili vya serikali vina mamlaka au majukumu kuyahusu.
(2)Sheria ya kitaifa itatawala juu ya sheria ya kaunti ikiwa—
(a)sheria za kitaifa inatumika kwa usawa kote nchini Kenya na masharti mengine yaliyowekwa katika ibara ya (3) yametoshelezwa; au
(b)sheria ya kitaifa inalenga kudhibiti hatua zisizofaa katika kaunti, ikiwa hatua hizo—
(i)zinaweza kuwa na athari mbaya kiuchumi, kiafya au katika usalama wa Kenya au kaunti nyingine; au
(ii)zitazuia utekelezaji wa sera ya kiuchumi ya kitaifa.
(3)Masharti yanayorejelewa katika ibara ya (2) (a) ni kama yafuatayo (2) (a)––
(a)sheria ya kitaifa inatoa mwongozo kuhusu suala ambalo haliwezi kudhibitiwa kwa ufanisi na sheria zitakazotungwa katika kila kaunti;
(b)sheria ya kitaifa inatoa mwongozo kuhusu suala ambalo linahitaji usawa kote nchini ili kutekelezwa kwa ufanisi, na sheria hiyo ya kitaifa inatoa usawa huo kwa kubuni—
(i)kanuni na viwango vya ubora; au
(ii)sera za kitaifa; au
(c)sheria hiyo ya kitaifa ni muhimu katika—
(i)kudumisha usalama wa kitaifa;
(ii)kudumisha umoja wa kiuchumi;;
(iii)kulinda soko la shirikisho katika usafirishaji wa bidhaa, huduma, rasilimali na wafanyakazi;
(iv)kukuza shughuli za kiuchumi katika mipaka ya kaunti;
(v)kukuza nafasi sawa au usawa katika ufikiaji wa huduma za serikali; au
(vi)kulinda mazingira.
(4)Sheria ya kaunti zitatawala juu ya sheria ya kitaifa ikiwa hali zote zinazobainiwa katika ibara ya (2) hazitumiki.
(5)Katika kutatua mgongano kati ya sheria za viwango tofauti vya serikali, mahakama itapendelea ufasiri wa sheria ambao utazuia mgongano badala ya ufasiri ambao utapelekea mgongano.
(6)Uamuzi wa mahakama kwamba kifungu cha sheria ya kiwango kimoja cha serikali kinatawala juu ya kifungu katika sheria ya kiwango kingine cha serikali hakubatilishi kifungu cha sheria cha kiwango kile kingine, ila tu kifungu hicho hakitatekelezwa kwa kiwango ambacho hakiambatani na kifungu kilichoamuliwa kutawala.