Ukuu wa Katiba Hii
(1)Katiba hii ndio sheria kuu ya Jamhuri na inapaswa kufuatwa na watu wote na idara zote za Serikali katika ngazi zote mbili za serikali.
(2)Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa na mamlaka au kutumia mamlaka ya Serikali ila tu kwa njia iliyoidhinishwa chini ya Katiba hii.
(3)Uhalali au uthabiti wa Katiba hii hauwezi kupingwa na au mbele ya mahakama yoyote au idara yoyote ya Serikali.
(4)Sheria yoyote, ikijumuisha sheria ya mila na tamaduni, ambayo haiambatani na Katiba hii ni batili kwa kiwango cha ukinzani huo, na tendo lolote au kutotenda kunakokiuka Katiba hii ni batili.
(5)Sheria za kijumla za kimataifa zitakuwa sehemu ya sheria za Kenya.
(6)Mkataba au maagano yoyote ambayo yataidhinishwa na Kenya yatakuwa sehemu ya sheria za Kenya chini ya Katiba hii.