Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nne · Sheria za Haki

Kifungu cha 20

Kif.20

Matumizi ya Sheria za Haki

(1)Sheria za Haki zinatumika katika sheria zote na ni lazima zifuatwe na idara zote za Serikali pamoja na watu wote.

(2)Kila mtu atafurahia haki na uhuru wa kimsingi zilizo katika Sheria za Haki kwa kiwango kikubwa iwezekanavyo, kulingana na hali ya haki hiyo au uhuru huo wa kimsingi.

(3)Katika kufasiri kifungu cha Sheria za Haki, mahakama—

(a)itakuza sheria kwa kiwango ambacho kitawezesha utekelezaji wa haki au uhuru wa kimsingi; na

(b)itachukua fasiri inayopendelea utekelezaji wa haki au uhuru wa kimsingi kwa kiwango kikubwa.

(4)Katika kufasiri Sheria za Haki, mahakama, taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama au mamlaka nyingine itakuza––

(a)maadili ya kimsingi katika jamii iliyo wazi na ya kidemokrasia, kwenye misingi ya hadhi ya binadamu, usawa na uhuru; na

(b)kusudi, madhumuni na malengo ya Sheria za Haki.

(5)Katika utekelezaji wa haki yoyote chini ya Kifungu cha 43, ikiwa Serikali itadai kwamba haina rasilimali za kutekelezea haki hiyo, mahakama, taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama au mamlaka nyingine itaongozwa na kanuni zifuatazo––

(a)ni jukumu la Serikali kuonesha kwamba rasilimali hazipatikani;

(b)katika kugawa rasilimali, Serikali itaweka kipaumbele jukumu la kuhakikisha kwamba kuna manufaa makubwa zaidi ya haki hiyo au uhuru huo wa kimsingi, kulingana na hali ilivyo, ikijumuisha unyonge wa vikundi fulani vya watu au watu binafsi; na

(c)mahakama, taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama au mamlaka nyingine haiwezi kuingilia uamuzi wa idara ya Serikali kuhusu ugavi wa rasilimali zinazopatikana, hasa kwenye misingi kwamba ingefikia uamuzi tofauti.

Isome ndani ya Sura ya Nne →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho