Hazina ya Usawazishaji
(1)Imebuniwa Hazina ya Usawazishaji ambayo itachukua asilimia ya nusu moja ya mapato yote yatakayokusanywa na serikali ya kitaifa katika kila mwaka, mapato hayo yakihesabiwa kwenye msingi wa akaunti zilizokaguliwa hivi majuzi kuhusu mapato yaliyokusanywa, kama ilivyoidhinishwa na Bunge la Kitaifa.
(2)Serikali ya kitaifa itatumia Hazina ya Usawazishaji kutoa huduma za kimsingi tu ikijumuisha maji, barabara, matibabu na nguvu za umeme katika maeneo yaliyotengwa kwa kiwango kitakachoboresha huduma hizo katika maeneo hayo ili ziwe sawa na viwango vya huduma vinavyotolewa katika maeneo mengine nchini, kama iwezekanavyo.
(3)Serikali ya kitaifa inaweza kutumia Hazina ya Usawazishaji––
(a)kwa kiasi tu ambacho matumizi ya fedha za hazina hiyo yameidhinishwa tu katika Mswada wa Matumizi ya Fedha uliopitishwa na Bunge; na
(b)kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kupitia kwa ruzuku zilizo na kwa kaunti ambazo zina jamii zilizotengwa.
(4)Ushauri wa Tume ya Ugavi wa Mapato utatafutwa na mapendekezo yake kuzingatiwa kabla ya Bunge kupitisha Mswada wowote unaoidhinisha matumizi ya fedha kutoka kwenye Hazina ya Usawazishaji.
(5)Fedha zozote katika Hazina ya Usawazishaji ambazo hazitakuwa zimetumiwa kufikia mwisho wa mwaka wa kifedha, zitasalia katika Hazina hiyo kwa matumizi kulingana na ibara ya (2) na (3) katika mwaka wa fedha utakaofuata.
(6)Kutekelezwa kwa Kifungu hiki kutamalizika miaka ishirini baada ya tarehe ya kuanza kutekelezwa kwa Katiba hii, lakini kwa kuzingatia ibara ya (7).
(7)Bunge linaweza kupitisha sheria itakayositisha utekelezaji wa ibara ya (6) kwa kipindi cha ziada cha miaka iliyowekwa, lakini kwa kuzingatia ibara ya (8).
(8)Sheria chini ya ibara ya (7) itaungwa na zaidi ya nusu ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, na zaidi ya nusu ya wajumbe wote wa kaunti katika Seneti.
(9)Fedha hazitaondolewa katika Hazina ya Usawazishaji isipokuwa Msimamizi wa Bajeti awe ameidhinisha kuondolewa huko.