Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Mbili · Fedha za Umma

Kifungu cha 206

Kif.206

Hazina ya jumla na hazina zingine za umma

(1)Hazina Jumuishi imebuniwa, ambayo itahifadhi fedha zilizozalishwa au kupokewa na, au kwa niaba ya serikali ya kitaifa, isipokuwa fedha ambazo—

(a)zimetengwa kutoka kwa Hazina hiyo kwa sababu maalum zilizotolewa na Sheria ya Bunge, na ambazo zitawekwa katika hazina nyingine ya umma iliyobuniwa kwa lengo maalum; au

(b)zinaweza, chini ya Sheria ya Bunge, kuhifadhiwa na kitengo cha Serikali kilichozipokea kwa lengo la kugharamia mahitaji ya kitengo hicho.

(2)Fedha zinaweza kuondolewa kutoka kwenye Hazina Jumuishi tu—

(a)kulingana na kuidhinishwa kwa matumizi yake kupitia kwa Sheria ya Bunge;

(b)kulingana na Kifungu cha 222 au 223; au

(c)kama malipo kutoka kwa Hazina hiyo kama ilivyoidhinishwa na Katiba hii au na Sheria ya Bunge.

(3)Fedha hazitaondolewa kwenye hazina nyingine yoyote ya fedha za umma kando na Hazina Jumuishi, isipokuwa kuondolewa kwa fedha hizo kumeidhinishwa na Sheria ya Bunge.

(4)Fedha hazitaondolewa kwenye Hazina Jumuishi isipokuwa Msimamizi wa Bajeti ameidhinisha kuondolewa huko.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Mbili →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho