Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nne · Sheria za Haki

Kifungu cha 22

Kif.22

Utekelezaji wa Sheria za Haki

(1)Kila mtu ana haki ya kuwasilisha kesi mahakamani akidai kwamba amenyimwa haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki, kwamba haki au uhuru huo umekiukwa au kutishiwa.

(2)Zaidi ya mtu kuwasilisha kesi kwa niaba yake mwenyewe, kesi chini ya sehemu ya (1) inaweza kuwasilishwa na––

(a)mtu anayewasilisha kesi kwa niaba ya mtu mwingine ambaye hawezi kuwasilisha kesi kwa jina lake mwenyewe;

(b)mtu anayewasilisha kesi kwa niaba ya, au kama mwanachama wa kikundi au tabaka la watu;

(c)mtu anayewasilisha kesi kwa manufaa ya umma; au

(d)shirika linalowasilisha kesi kwa manufaa ya mwanachama mmoja au zaidi.

(3)Jaji Mkuu atatunga kanuni zitakazotoa mwongozo katika kesi zilizorejelewa katika Kifungu hiki, ambazo zitatimiza vigezo kwamba––

(a)haki za kuwasilisha kesi zilizotolewa katika sehemu ya (2) zinatekelezwa kikamilifu;

(b)hali rasmi zinazohusiana na kesi hizo, ikijumuisha kuanzishwa kwa kesi, unawekwa kwa kiwango cha chini, na hasa kwamba iwapo ni muhimu, mahakama itakubali kuendeshwa kwa kesi kwenye msingi wa hati na rekodi zisizo rasmi;

(c)hakuna ada itakayotozwa kwa kuanzisha kesi;

(d)kwa kuzingatia kanuni za haki ya kimsingi, mahakama haitazuiwa na mahitaji madogo madogo ya utaratibu; na

(e)shirika au mtu binafsi mwenye ujuzi maalum anaweza, kwa idhini ya mahakama, kujitokeza kama msaidizi wa mahakama katika kutatua maswala ya kisheria.

(4)Kukosekana kwa kanuni zinazoangaziwa katika sehemu ya (3) hakutadhibiti haki ya mtu yeyote ya kuwasilisha kesi mahakamani chini ya Kifungu hiki, na mahakama kuisikiza na kuiamua kesi hiyo.

Isome ndani ya Sura ya Nne →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho