Udhibiti wa fedha
(1)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu kubuniwa kwa Hazina ya kitaifa, majukumu na uwajibikaji wa Hazina hiyo.
(2)Bunge litatunga sheria ili kuhakikisha kuwa kunausimamizi wa matumizi na uwajibikaji katika serikali zote na litaweka mikakati ili kuhakikisha kwamba usimamizi huo na uwajibikaji umetekelezwa.
(3)Sheria chini ya ibara ya (2) inaweza kumwidhinisha Waziri anayehusika na fedha kusitisha uhamishaji wa fedha kwa kitengo fulani cha Serikali au shirika lolote la umma—
(a)iwapo tu kuna ukiukaji mkubwa au ukiukaji wa mara kwa mara wa hatua zilizowekwa chini ya sheria hiyo; na
(b)kwa kuzingatia mahitaji ya ibara ya (4) hadi ya (7).
(4)Uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha chini ya ibara ya (3) hauwezi kusitisha uhamishaji wa zaidi ya asilimia hamsini ya fedha zinazopaswa kuhamishwa kwa serikali ya kaunti.
(5)Uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha, unavyobainishwa chini ya ibara ya (3)—
(a)hautasitisha kuhamishwa kwa fedha kwa zaidi ya siku sitini; na
(b)unaweza kutekelezwa mara moja, lakini unaweza kuwacha kutekelezwa kwa mtazamo wa muda uliopita isipokuwa katika muda wa siku thelathini baada ya tarehe ya uamuzi huo, Bunge liidhinishe kwa uamuzi utakaopitishwa katika ngazi zote mbili za Bunge.
(6)Bunge linaweza kuweka upya uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha, lakini kwa siku zisizozidi sitini kwa wakati mmoja.
(7)Bunge haliwezi kuidhinisha au kuweka upya uamuzi wa kusitisha uhamishaji wa fedha isipokuwa—
(a)Msimamizi wa Bajeti amewasilisha ripoti kuhusu suala hilo Bungeni; na
(b)shirika hilo la umma limepewa nafasi ya kujibu madai dhidi yake, na kujitetea mbele ya kamati husika ya bunge.