Ununuaji wa bidhaa na huduma za umma
(1)Kitengo cha serikali au shirika lolote la umma linapotoa kandarasi za ununuzi wa bidhaa au huduma, shirika au kitengo hicho kitafanya hivyo kulingana na mfumo ambao ni wa haki, wenye usawa, uwazi, wenye ushindani na wenye bei nafuu.
(2)Sheria ya Bunge itatoa mwongozo kuhusu jinsi sera zinazohusiana na ununuzi na uuzaji wa mali zitavyotekelezwa na inaweza kutoa mwongozo kuhusu suala moja au masuala yote—
(a)kategoria za kupewa kipaumbele wakati wa kutoa kandarasi;
(b)ulinzi au maendeleo ya watu, kategoria za watu au vikundi vya watu ambao walinyanyaswa kwa ushindani usio wa haki au uliowabagua na kuwatenga hapo awali;
(c)adhabu dhidi ya wanakandarasi ambao utendakazi wao hautimizi viwango vilivyokubaliwa kitaaluma, makubaliano ya kimkataba au sheria; na
(d)adhabu dhidi ya watu ambao hawajalipa kodi au ushuru, au ambao wamehusika katika ufisadi au ambao wamekiuka vikubwa sheria kuhusu uajiri wa haki.