Mkaguzi Mkuu wa Serikali
(1)Kutakuwa na Mkaguzi Mkuu atakayependekezwa na Rais, na kwa idhini ya Bunge la Kitaifa, kuteuliwa na Rais.
(2)Ili kustahiki kuwa Mkaguzi Mkuu, lazima mtu awe na ufahamu mkubwa katika masuala ya fedha za umma, au uzoefu wa muda usiopungua miaka kumi katika ukaguzi au usimamizi wa fedha za umma.
(3)Kwa kuzingatia Kifungu cha 251, Mkaguzi Mkuu atahudumu kwa muhula wa miaka nane na hatastahiki kuteuliwa tena.
(4)Katika muda wa miezi sita baada ya kukamilika kwa kila mwaka wa kifedha, Mkaguzi Mkuu, kwa madhumuni ya mwaka huo wa kifedha, atakagua na kuripoti kuhusu masuala yafuatayo—
(a)hesabu za serikali ya kitaifa na serikali za kaunti;
(b)hesabu za hazina zote na mashirika ya serikali ya kitaifa na ya serikali za kaunti;
(c)hesabu za mahakama zote;
(d)hesabu za kila tume na ofisi huru zilizobuniwa chini ya Katiba hii;
(e)hesabu za Bunge la Kitaifa, Seneti na mabunge ya kaunti;
(f)hesabu za fedha za vyama vya kisiasa ambazo zinatoka katika hazina za umma.
(g)deni la umma; na
(h)hesabu za shirika lingine lolote ambalo linatakiwa kisheria kufanyiwa ukaguzi na Mkaguzi Mkuu.
(5)Mkaguzi Mkuu anaweza kukagua na kutoa ripoti kuhusu hesabu za shirika lolote linalopokea fedha kutoka kwenye hazina za umma.
(6)Ripoti ya ukaguzi itathibitisha iwapo fedha za umma zimetumiwa kwa mujibu wa sheria na kwa njia yenye ufanisi.
(7)Ripoti za ukaguzi zitawasilishwa katika Bunge au katika bunge la kaunti.
(8)Katika muda wa miezi mitatu baada ya kupokea ripoti ya ukaguzi, Bunge la Kitaifa au la kaunti litazingatia na kujadili ripoti hiyo na kuchukua hatua ifaayo.