Mamlaka na Kazi ya Tume ya Huduma kwa Umma
(1)Majukumu na mamlaka ya Tume ni kama yalivyoelezwa katika Kifungu hiki.
(2)Tume—
(a)kwa kuzingatia Katiba hii na sheria––
(i)itabuni na kuondoa nafasi za kuhudumu katika huduma za umma; na
(ii)itateua watu watakaohudumu katika ofisi hizo, na itathibitisha uteuzi;
(b)itadumisha nidhamu na kuwaondoa kazini watu wanaohudumu katika ofisi hizo au walioteuliwa ili kuhudumu kwa muda mfupi;
(c)itakuza maadili na kanuni zilizotajwa katika Vifungu vya 10 na 232 kote katika utoaji wa huduma za umma;
(d)itachunguza, kufuatilia, na kutathmini mipangilio, usimamizi na mienendo ya wafanyakazi walio katika huduma za umma;
(e)itahakikisha huduma za umma ni zenye ufanisi na bora;
(f)itakuza uwezo wa wafanyakazi katika huduma za umma;
(g)itachunguza na kutoa mapendekezo kwa serikali ya kitaifa kuhusu hali za utendakazi, kanuni za maadili na ustahiki wa maafisa walio katika huduma za umma;
(h)itatathmini na kuripoti kwa Rais na Bunge kuhusu kiwango ambacho maadili na kanuni zilizotajwa katika Vifungu vya 10 na 232 zinazingatiwa katika huduma za umma;
(i)itasikiza na kuamua maombi kuhusu masuala yanayohusiana na huduma za umma katika serikali za kaunti;
(j)itatekeleza majukumu na mamlaka mengine yoyote kama yatakavyotolewa na sheria ya kitaifa.
(3)Ibara za (1) na (2) hazitatumika katika ofisi zozote kati ya zifuatazo, zilizo katika huduma za umma––
(a)ofisi za Serikali;
(b)ofisi ya kamishna mkuu, balozi au mwakilishi yeyote wa kidiplomasia katika Jamhuri;
(c)ofisi au wadhifa ulio chini ya––
(i)Tume ya Huduma za Bunge;
(ii)Tume ya Huduma za Mahakama;
(iii)Tume ya Huduma kwa Walimu;
(iv)Tume ya Huduma za Kitaifa za Polisi; au
(b)ofisi inayohudumia serikali ya kaunti, isipokuwa ilivyobainiwa katika ibara ya (2) (i).
(4)Tume haitamteua mtu chini ya ibara ya (2) ili kuhudumu au kutoa huduma kwa muda mfupi katika ofisi yoyote iliyo kati ya wafanyakazi wa kibinafsi wa Rais au Rais mstaafu, isipokuwa kwa idhini ya Rais au Rais mstaafu huyo.
(5)Kupitia kwa njia ya maandishi, Tume inaweza, kwa masharti au bila ya masharti, kukabidhi majukumu na mamlaka yake yoyote chini ya Kifungu hiki kwa mwanachama au wanachama wake, au kwa afisa yeyote, shirika au mamlaka katika huduma za umma.