Udhibiti wa haki au uhuru wa kimsingi
(1)Haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki hazitadhibitiwa isipokuwa kulingana na sheria, na kwa kiwango ambacho kinafaa katika jamii iliyo wazi na ya kidemokrasia, na iliyo kwenye misingi ya hadhi ya binadamu, usawa na uhuru, na kwa kuzingatia maswala yote husika ikijumuisha––
(a)hali ya haki hiyo au uhuru huo wa kimsingi;
(b)umuhimu wa lengo la udhibiti huo;
(c)hali na kiwango cha udhibiti huo;
(d)umuhimu wa kuhakikisha kwamba kutekelezwa kwa haki hizo na uhuru huo wa kibinafsi wa mtu yeyote hautatizi haki na uhuru wa kimsingi wa watu wengine; na
(e)uhusiano kati ya udhibiti huo na lengo lake, na ikiwa kuna njia zingine ambazo hazidhibiti sana na ambazo zinaweza kufikia lengo hilo.
(2)Licha ya sehemu ya (1), kifungu katika sheria kinachodhibiti haki au uhuru wa kimsingi—
(a)ikiwa ni kifungu kilichotungwa au kurekebishwa katika, au baada ya siku ya kuanza kutumika kwa Katiba hii, kifungu hicho sio halali, isipokuwa sheria hiyo idhihirishe kusudi la kudhibiti haki hiyo au uhuru huo wa kimsingi na kiwango cha udhibiti huo;
(b)hakitachukuliwa kuwa kinadhibiti haki hiyo au uhuru huo isipokuwa kieleze wazi na kwa njia maalum kuhusu haki au uhuru wa kimsingi unaodhibitiwa na hali au kiwango cha udhibiti huo; na
(c)hakitadhibiti haki au uhuru wa kimsingi kwa njia itakayotofautiana na maudhui muhimu ya haki au uhuru huo wa kimsingi.
(3)Serikali au mtu anayetaka kuhalalisha udhibiti fulani atathibitishia mahakama, taasisi iliyo na mamlaka ya mahakama au mamlaka nyingine kwamba mahitaji ya Kifungu hiki yameridhishwa.
(4)Vifungu katika Sura hii kuhusu usawa vitadhibitiwa katika utekelezaji wa Sheria ya Kiislamu katika mahakama za Kadhi kwa waumini wa dini ya Kiislamu, katika maswala yanayohusiana na hadhi zao za kibinafsi, hali ya ndoa, talaka na urithi.
(5)Licha ya sehemu za (1) na (2), kifungu katika sheria kinaweza kudhibiti utekelezaji wa haki na uhuru wa kimsingi katika vifungu vifuatavyo, kwa watu wanaohudumu katika Majeshi ya Ulinzi ya Kenya au Huduma ya Kitaifa ya Polisi–
(a)31—Faragha;
(b)36—Uhuru wa kutangamana;
(c)37—Mikutano, maandamano, migomo na maombi;
(d)41—Mahusiano ya kikazi;
(e)43—Haki za kiuchumi na za kijamii; na
(f)49—Haki za waliotiwa mbaroni.