Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Tano · Tume na Ofisi Huru

Kifungu cha 250

Kif.250

Muundo, uteuzi na muda wa kuwa ofisini

(1)Kila tume itakuwa na angalau wanachama watatu, lakini wasiozidi tisa.

(2)Mwenyekiti na kila mwanachama wa tume, pamoja na anayehudumu katika ofisi huru—

(a)watatambuliwa na kupendekezwa ili wateuliwe kwa namna iliyoagizwa na sheria ya kitaifa;

(b)wataidhinishwa na Bunge la Kitaifa; na

(c)watateuliwa na Rais.

(3)Ili kuteuliwa, mtu atapaswa kuwa na ustahiki maalum unaohitajika na Katiba hii au sheria ya kitaifa.

(4)Uteuzi wa wanachama wa tume na wa maafisa wa ofisi huru utazingatia maadili ya kitaifa yanayorejelewa katika Kifungu cha 10, na kanuni kwamba uanachama wa tume na wanaohudumu katika ofisi huru, kijumla, utaonyesha utofauti wa kimaeneo na kikabila wa wananchi wa Kenya.

(5)Mwanac hama wa t u m e anawe z a kuhudumu kwa muda.

(6)Mwanachama wa tume au anayehudumu katika ofisi huru—

(a)isipokuwa awe na uanachama usio rasmi, atateuliwa kwa muhula mmoja wa miaka sita, na hastahiki kuteuliwa tena; na

(b)isipokuwa awe na uanachama usio rasmi au awe anahudumu kwa muda, mtu huyo hatahudumu katika ofisi nyingine au kuajiriwa ili kupokea mapato, katika ofisi ya umma au ya kibinafsi.

(7)Malipo na marupurupu atakayopata kamishna au anayehudumu katika ofisi huru, yatalipwa kutoka kwenye Hazina Jumuishi.

(8)Malipo na marupurupu atakayopata kamishna au anayehudumu katika ofisi huru hayatabadilishwa na kupelekea hasara kwa mtu huyo.

(9)Mwanachama wa tume au anayehudumu katika ofisi huru hatawajibika kisheria kwa jambo lolote lililofanywa kwa nia njema katika utekelezaji wa jukumu la ofisi hiyo.

(10)Wanachama wa tume watamchagua naibu mwenyekiti kutoka miongoni mwao—

(a)katika kikao cha kwanza cha tume; na

(b)kila inapohitajika kujaza nafasi katika ofisi ya naibu mwenyekiti.

(11)Mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa tume hawatakuwa wa jinsia moja.

(12)Kutakuwa na Katibu wa kila tume, ambaye—

(a)atateuliwa na tume; na

(b)afisa mkuu mtendaji wa tume hiyo.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Tano →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho