Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Kumi na Saba · Vifungu vya Kijumla

Kifungu cha 259

Kif.259

Kufasiri Katiba Hii

(1)Katiba hii itafasiriwa kwa namna ambayo—

(a)inakuza malengo, maadili na kanuni zake;

(b)inaendeleza utawala wa sheria, haki za binadamu na uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki;

(c)inaruhusu kuendelea kwa sheria; na

(d)inachangia katika utawala bora.

(2)Ikiwa kuna mgongano kati ya matoleo ya Katiba hii katika lugha tofauti, toleo la lugha ya Kiingereza ndilo litakalotawala.

(3)Kila kifungu katika Katiba hii litafasiriwa kulingana na kanuni ya ufasiri kwamba sheria inazungumza kila mara, na kwa hivyo, kati ya masuala mengine—

(a)jukumu au mamlaka yaliyotolewa na Katiba hii kwa ofisi yanaweza kutekelezwa na mtu anayehudumu katika ofisi hiyo kulingana na hitaji;

(b)rejeleo lolote katika Katiba hii kwa Serikali au ofisi nyingine ya umma au afisa, au mtu anayehudumu katika ofisi hiyo ni rejeleo kwa mtu anayehudumu katika ofisi hiyo kwa muda au anayetekeleza majukumu ya ofisi hiyo kwa wakati wowote ule;

(c)rejeleo katika Katiba hii kwa ofisi, kitengo cha Serikali au eneo lililotajwa katika Katiba hii litasomwa kwa kuzingatia badiliko lolote rasmi linalohitajika ili liweze kutumika katika hali hizo; na

(d)rejeleo katika Katiba hii kwa ofisi au shirika, ikiwa ofisi au shirika hilo halipo tena, ni rejeleo kwa ofisi au shirika lililorithi, au ofisi au shirika sawa na lile ambalo halipo tena.

(4)Katika Katiba hii, isipokuwa pale ambapo muktadha unahitaji vinginevyo—

(a)iwapo neno au maelezo yamefafanuliwa katika Katiba hii, tofauti zozote za kisarufi au za kimatumizi ya neno linalohusiana na jingine, soma ukizingatia mabadiliko yanayotokana na muktadha; na

(b)neno “ikijumuisha” linamaanisha “ikijumuisha, lakini bila kudhibiti”.

(5)Katika kuhesabu muda uliopita kati ya matukio mawili, kwa madhumuni yoyote chini ya Katiba hii, ikiwa muda huo umeelezwa—

(a)kama siku, basi siku ambayo tukio la kwanza linatokea haitahesabiwa, na siku ambayo tukio la mwisho linaweza kutokea itajumuishwa;

(b)kama miezi, kipindi cha muda uliowekwa unaisha mwanzoni mwa siku katika mwezi husika—

(i)ambayo ina nambari sawa kama tarehe ambayo kipindi hicho kilianza, ikiwa mwezi huo una tarehe inayolingana; au

(ii)ndiyo siku ya mwisho ya mwezi huo, katika hali yoyote nyingine; au

(c)kama miaka, kipindi cha muda huo kinamalizika mwanzoni mwa tarehe ya mwaka husika inayolingana na tarehe ambayo kipindi hicho kilianza.

(6)Ikiwa muda uliowekwa katika Katiba hii kwa madhumuni yoyote ni siku sita au chini yake, Jumapili na siku za mapumziko za kitaifa hazitahesabiwa muda huo unapohesabiwa.

(7)Ikiwa katika hali zozote maalum, kipindi cha muda kilichowekwa na Katiba hii kinakamilika siku ya Jumapili au siku ya mapumziko ya kitaifa, muda huo unaongezwa hadi siku inayofuata ambayo sio Jumapili au siku ya mapumziko ya kitaifa.

(8)Ikiwa muda fulani haujawekwa na Katiba hii katika utekelezaji wa kitendo fulani, kitendo hicho kitafanywa bila kuchelewa kusio na sababu za kuridhisha, na kulingana na itakavyohitajika mara kwa mara.

(9)Ikiwa mtu yeyote au kitengo cha Serikali kina mamlaka chini ya Katiba hii ya kuongeza kipindi cha muda uliowekwa na Katiba hii, mamlaka hayo yanaweza kutekelezwa kabla au baada ya mwisho wa kipindi hicho, isipokuwa pale ambapo nia tofauti imeelezewa wazi katika kifungu kinachotoa mamlaka hayo.

(10)Isipokuwa pale ambapo Katiba hii inaelezea vinginevyo, ikiwa mtu ameondoka katika ofisi iliyobuniwa chini ya Katiba hii, ikiwa mtu huyo anastahiki, anaweza kuteuliwa tena, kuchaguliwa au vinginevyo kuteuliwa ili kuhudumu katika ofisi hiyo kulingana na Katiba hii.

(11)Ikiwa jukumu au mamlaka yaliyotolewa kwa mtu chini ya Katiba hii yanaweza kutekelezwa na mtu huyo tu kupitia kwa ushauri au pendekezo, kupitia kwa idhini ya mtu mwingine au mashauriano na mtu mwingine, jukumu hilo linaweza kufanywa au mamlaka hayo kutekelezwa kupitia tu kwa ushauri huo, pendekezo, idhini au baada ya mashauriano hayo, isipokuwa kwa kiwango ambacho Katiba hii inatoa mwongozo vinginevyo.

Isome ndani ya Sura ya Kumi na Saba →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho