Usawa na uhuru kutokana na ubaguzi
(1)Kila mtu ni sawa mbele ya sheria, na ana haki ya kulindwa na kupata manufaa sawa ya sheria.
(2)Usawa unajumuisha kufurahia haki zote na uhuru wote wa kimsingi kikamilifu na kwa usawa.
(3)Wanawake na wanaume wana haki ya kuchukuliwa kwa usawa ikijumuisha haki ya kupata nafasi sawa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kitamaduni na kijamii.
(4)Serikali haitabagua mtu yeyote kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kwenye misingi yoyote ikijumuisha asili, jinsia, ujauzito, hali ya mtu kindoa, hali ya kiafya, asili ya kikabila au kijamii, rangi, umri, ulemavu, dini, dhamira, imani, utamaduni, mavazi, lugha au kuzaliwa.
(5)Mtu hatambagua mtu mwingine kwa njia ya moja kwa moja au vinginevyo kwenye misingi iliyotajwa au kuelezewa katika ibara ya (4).
(6)Ili kuwezesha utekelezaji kamili wa haki zilizohakikishwa chini ya Kifungu hiki, Serikali itachukua hatua za kisheria na nyinginezo, ikijumuisha programu na sera za vitendo sawazishi ambazo zimebuniwa ili kusawazisha upungufu wowote uliowaathiri watu binafsi au vikundi vya watu kwa sababu ya ubaguzi wa hapo awali.
(7)Hatua yoyote inayochukuliwa chini ya ibara ya (6) itazingatia kikamilifu ili manufaa yoyote yawe kwenye msingi wa hitaji la kweli.
(8)Zaidi ya hatua zinazokusudiwa katika sehemu ya (6), Serikali itachukua hatua za kisheria na nyinginezo ili kutekeleza kanuni inayohitaji kwamba idadi ya watu waliochaguliwa au kuteuliwa katika mashirika yanayoteua au ambayo yanahitaji watu kuchaguliwa haitakuwa na idadi ya jinsia moja inayozidi thuluthi mbili.