Haki za kisiasa
(1)Kila mwananchi ana uhuru wa kumchagua mtu amtakaye kisiasa, ikijumuisha haki ya—
(a)kuunda, au kushiriki katika uundaji wa chama cha kisiasa;
(b)kushiriki katika shughuli za chama cha kisiasa, au kusajili wanachama kwa niaba ya chama cha kisiasa; au
(c)kupigia kampeni chama cha kisiasa au madhumuni ya kisiasa.
(2)Kila raia ana haki ya kushiriki katika uchaguzi huru, wa haki na unaofanyika mara kwa mara kwenye msingi wa haki ya kupiga kura kwa wote, na uhuru wa wapiga kura kueleza matakwa yao katika—
(a)shirika au ofisi yoyote ya umma ambayo wanachama wake huchaguliwa na iliyoundwa chini ya Katiba; au
(b)ofisi yoyote au chama chochote cha kisiasa ambacho raia huyo ni mwanachama.
(3)Bila kudhibitiwa kiholela, kila raia mwenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi ana haki ya—
(a)kusajiliwa kama mpiga kura;
(b)kupiga kura ya siri katika uchaguzi wowote au katika kura ya maamuzi; na
(c)kugombea wadhifa katika ofisi ya umma, au ofisi katika chama cha kisiasa ambacho raia huyo ni mwanachama na ikiwa atachaguliwa, kutekeleza majukumu ya ofisi hiyo.