Ulinzi wa haki ya kumiliki mali
(1)Kwa kuzingatia Kifungu cha 65, kila mtu ana haki, kibinafsi au kwa kuungana na wengine, kupata na kumiliki mali––
(a)ya aina yoyote; na
(b)katika sehemu yoyote ya Kenya.
(2)Bunge halitatunga sheria inayoruhusu Serikali au mtu yeyote—
(a)kwa udhalimu kumpokonya mtu mali ya aina yoyote au kumnyima mtu haki yake katika mali ya aina yoyote;
(b)kumzuia, au kwa njia yoyote kumzuia kufurahia haki yoyote chini ya Kifungu hiki kwenye misingi iliyobainishwa au kutajwa katika Kifungu cha (27) (4).
(3)Serikali haitamzuia mtu kumiliki mali ya aina yoyote, au kuwa na haki katika mali ya aina yoyote isipokuwa kuzuiwa huko—
(a)kunatokana na upataji ardhi au manufaa fulani katika ardhi au ubadilishaji wa manufaa fulani ya ardhi au hatimiliki ya ardhi, kulingana na Sura ya Tano; au
(b)ni kwa matumizi ya umma au ni kwa manufaa ya umma na kunatekelezwa kulingana na Katiba hii na Sheria yoyote ya Bunge ambayo—
(i)inahakikisha malipo ya fidia na ya haki kikamilifu kwa mtu huyo; na
(ii)inampa mtu yeyote aliye na manufaa au haki katika mali hiyo haki ya kufikia mahakama ya kisheria.
(4)Sheria hiyo inaweza kuruhusu wakazi wa ardhi iliyopatikana kulingana na sehemu ya (3), ambao huenda hawana hatimiliki ya ardhi hiyo, kufidiwa kwa nia njema.
(5)Serikali itatoa msaada, itakuza na kulinda hakimiliki ya uvumbuzi wa wananchi wa Kenya.
(6)Haki chini ya Kifungu hiki hazijumuishi mali yoyote ambayo ilipatikana kwa njia isiyo halali.