Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Nne · Sheria za Haki

Kifungu cha 49

Kif.49

Haki za watu waliotiwa mbaroni

(1)Mtu aliyekamatwa ana haki ya—

(a)kuarifiwa mara moja na kupitia kwa lugha anayoielewa, kuhusu—

(i)sababu ya kukamatwa;

(ii)haki ya kunyamaza kimya; na

(iii)matokeo ya kutonyamaza kimya;

(b)kunyamaza kimya;

(c)kuwasiliana na wakili na watu wengine ambao msaada wao unahitajika;

(d)kutolazimishwa kukiri au kukubali hatia, ambako kukubali huko kunaweza kutumiwa kama ushahidi dhidi ya mtu huyo;

(e)kutenganishwa na watu wanaotumikia vifungo vyao;

(f)kuletwa mahakamani haraka iwezekanavyo, lakini sio baada ya––

(i)saa ishirini na nne baada ya kukamatwa; au

(ii)ikiwa saa hizo ishirini na nne zimekamilika kwa wakati ambapo vikao vya mahakama haviendelei, au kwa siku isiyo ya mahakama, afikishwe mahakamani ifikapo mwisho wa siku ya mahakama inayofuata;

(g)afikishwapo mahakamani kwa mara ya kwanza, kufunguliwa mashtaka au kuarifiwa kuhusu sababu ya kuendelea kuzuiliwa kwake, au kuachiliwa huru; na

(h)kuachiliwa kwa dhamana, na kuwekewa masharti yanayoeleweka kabla ya kushtakiwa au kabla ya kesi kusikizwa, isipokuwa kukiwa na sababu zingine za kutomwachilia.

(2)Mtu hatazuiliwa katika rumande kwa kosa ikiwa kosa hilo linaweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini pekee au kwa kufungwa gerezani kwa muda usiozidi miezi sita.

Isome ndani ya Sura ya Nne →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho