Hali ya hatari
(1)Hali ya dharura inaweza kutangazwa tu chini ya Kifungu cha 132 (4) (d) na wakati ambapo––
(a)Nchi inatishiwa na vita, uvamizi, upinzani kijumla,
(b)vurugu, janga la kiasili au dharura nyingine ya umma; na
(c)tangazo hilo ni muhimu ili kukabili hali ambayo imesababisha kutolewa kwa tangazo hilo la dharura.
(2)Tangazo la hali ya dharura, na sheria yoyote itakayotungwa au hatua nyingine itakayochukuliwa kutokana na tangazo hilo, litafaa tu—
(a)ikiwa linalingana na matarajio; na
(b)kwa muda usiozidi siku kumi na nne kuanzia siku ya kutangazwa kwa hali hiyo ya dharura, isipokuwa Bunge la Kitaifa liamue kuendeleza tangazo hilo.
(3)Bunge la Kitaifa linaweza kuendeleza tangazo la hali ya hatari —
(a)kwa uamuzi uliokubaliwa—
(i)kufuatia mjadala wa wazi katika Bunge la Kitaifa; na
(ii)na idadi kubwa ya wabunge kama ilivyoelezewa katika sehemu ya (4); na
(b)kwa muda usiozidi miezi miwili kwa wakati mmoja.
(4)Kuongezwa kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha hali ya dharura kunahitaji kura ya uungwaji mkono ya angalau thuluthi mbili ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa, na kuongezwa kwa muda huo kwa mara nyingine kutahitaji kura ya uungwaji mkono ya angalau robo tatu ya wabunge wote katika Bunge la Kitaifa.
(5)Mahakama ya Juu Zaidi inaweza kuamua kuhusu uhalali wa—
(a)tangazo la hali ya dharura;
(b)kuongezwa kwokwote kwa muda wa tangazo la hali ya dharura;na
(c)sheria yoyote itakayotungwa au hatua yoyote nyingine itakayochukuliwa kwa sababu ya tangazo la hali ya dharura.
(6)Sheria yoyote inayotungwa kwa sababu ya tangazo la hali ya dharura––
(a)inaweza kudhibiti haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria za Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa ya Kenya. Haki kwa kiwango tu ambacho—
(i)udhibiti huo unahitajika haswa katika dharura hiyo; na
(ii)sheria hiyo inaambatana na majukumu ya Jamhuri chini ya sheria za kimataifa zinazotumika katika hali ya dharura; na
(b)haitatekelezwa hadi itakapochapishwa kwenye Gazeti Rasmi la Serikali.
(7)Tangazo la hali ya dharura au sheria inayotungwa au hatua yoyote nyingine inayochukuliwa kwa sababu ya tangazo lolote haitaruhusu au kuidhinisha ulinzi dhidi ya mashtaka kwa Serikali au mtu yeyote, katika tendo lolote la ukiukaji wa sheria.