Tume ya Kitaifa ya Haki za Binadamu na Usawa
(1)Tume ya Kitaifa ya Kenya ya Haki za Binadamu na Usawa ya Kenya Imebuniwa.
(2)Majukumu ya Tume hii ni—
(a)kukuza heshima ya haki za binadamu na kuendeleza desturi ya kuheshimu haki za binadamu katika Jamhuri;
(b)kukuza usawa wa kijinsia na usawa kijumla na kuratibu na kuhakikisha jinsia imezingatiwa katika maendeleo ya kitaifa;
(c)kukuza ulinzi na kuzingatiwa kwa haki za binadamu katika taasisi za umma na za kibinafsi;
(d)kufuatilia, kuchunguza na kuripoti jinsi haki za binadamu zinavyozingatiwa katika nyanja zote za kitaifa ikijumuisha jinsi idara za usalama wa kitaifa zinavyozingatia haki hizo;
(e)kupokea na kuchunguza malalamishi kuhusu tuhuma za ukiukaji wa haki na kuchukua hatua za kupata suluhisho lifaalo pale ambapo haki za binadamu zimekiukwa;
(f)kwa juhudi zake au kwenye msingi wa malalamishi, kuchunguza au kutafiti kuhusu suala la haki za binadamu, na kutoa mapendekezo ya kuimarisha utendakazi wa idara za Serikali;
(g)kutenda kama idara kuu ya Serikali katika kuhakikisha kuwa majukumu chini ya mikataba na maagano yanayohusiana na haki za binadamu yamefikiwa;
(h)kuchunguza mienendo yoyote katika masuala ya serikali, au matendo yoyote katika utawala wa umma na katika nyanja zozote za serikali yanayotuhumiwa au kushukiwa kutokuwa ya haki au kutofaa, au kupelekea hali isiyofaa au kutotendeka kwa haki;
(i)kuchunguza malalamishi yoyote kuhusu matumizi mabaya ya mamlaka, matendo yasiyo ya haki, kutotendeka kwa haki au mienendo rasmi isiyokuwa na usawa, inayonyanyasa au isiyoshughulika ipasavyo;
(j)kuripoti malalamishi yaliyochunguzwa chini ya aya za (h) na (i) na kuchukua hatua zinazofaa; na
(k)kutekeleza majukumu mengine yoyote yalioagizwa na sheria.
(3)Kila mtu ana haki ya kuilalamikia Tume akidai kwamba amenyimwa haki au uhuru wa kimsingi katika Sheria za Haki, kwamba haki au uhuru wa kimsingi umekiukwa, umevunjwa au kutishiwa.
(4)Bunge litatunga sheria ili kuwezesha kikamilifu utekelezaji wa Sehemu hii, na sheria nyingine yoyote kama hiyo inaweza kupanga upya Tume hiyo iwe tume mbili au zaidi tofauti.
(5)Ikiwa Bunge litatunga sheria ya kupanga upya Tume chini ya sehemu ya (4)––
(a)sheria hiyo itagawa kila jukumu la Tume iliyotajwa katika Kifungu hiki kwa tume moja au nyingine zinazobuniwa;
(b)kila mojawapo ya tume hizi zilizobuniwa itakuwa na mamlaka sawa na ile ya Tume iliyo chini ya Kifungu hiki; na
(c)kila tume itakayobuniwa itakuwa tume katika ufafanuzi wa Sura ya Kumi na Tano, na itakuwa na hadhi na mamlaka ya tume chini ya Sura hiyo.