Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tano · Ardhi na Mazingira

Kifungu cha 62

Kif.62

Ardhi ya umma

(1)Ardhi ya umma ni—

(a)ardhi ambayo ilikuwa inamilikiwa na serikali na ambayo haikuwa imegawanywa wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii, kama ilivyoelezewa na Sheria ya Bunge wakati iliyokuwa ikitumika wakati wa kuanza kutumika kwa Katiba hii;

(b)ardhi inayomilikiwa, kutumiwa au ambapo idara yoyote ya Serikali inapofanyia kazi, isipokuwa ardhi ambayo idara ya Serikali imekodisha kama mkodishaji wa kibinafsi;

(c)ardhi iliyokabidhiwa Serikali kwa njia ya kuuzwa, kurudishwa au kusalimishwa;

(d)ardhi ambayo umiliki wake wa kijamii au kibinafsi hauwezi kuthibitishwa kupitia mchakato wowote wa kisheria;

(e)ardhi ambayo hakuna mrithi yeyote anayeweza kutambuliwa kupitia mchakato wowote wa kisheria;

(f)ardhi yoyote iliyo na madini au mafuta ya madini kama ilivyoelezewa kisheria;

(g)misitu ya serikali isipokuwa misitu inayotajwa katika Kifungu cha hifadhi za wanyama, chemichemi za maji, mbuga za kitaifa, hifadhi za wanyama za serikali na maeneo maalum yaliyolindwa;

(h)barabara zote kulingana na Sheria ya Bunge;

(i)mito yote, maziwa yote na sehemu zingine za maji kama ilivyoelezewa na Sheria ya Bunge;

(j)mipaka ya bahari, maeneo maalum ya kiuchumi katika bahari na ardhi iliyo chini ya bahari;

(k)Ardhi iliyo chini ya bahari lakini kwenye upande wa bahari usio kuwa wenye kina sana;

(l)Ardhi yote iliyo kati ya nyanda za juu na za chini za maji;

(m)ardhi yoyote ambayo haijaainishwa kama ya kibinafsi au ya jamii chini ya Katiba hii; na

(n)ardhi yoyote iliyotangazwa kuwa ya umma kupitia kwa Sheria ya Bunge—

(i)Iliyokuwa ikitumika katika tarehe ya kuanza kutumika kwa katiba hii; au

(ii)iliyotungwa baada ya tarehe ya kuanza kutumika kwa katiba hii.

(2)Ardhi ya umma itamilikiwa na serikali ya kaunti kwa niaba ya wakazi katika kaunti hiyo, na itasimamiwa kwa niaba yao na Tume ya Kitaifa ya Ardhi ikiwa imeainishwa chini ya—

(a)sehemu ya ibara ya (1) (a), (c), (d) au (e); na

(b)sehemu ya (1) (b), isipokuwa ardhi ambayo inamilikiwa au inatumiwa na idara ya Serikali, au ambapo idara ya Serikali inafanyia kazi.

(3)Ardhi ya umma iliyoainishwa chini ya sehemu ya (1) (f) hadi (m) itamilikiwa na serikali ya kitaifa kwa niaba ya Wakenya na Tume ya Kitaifa ya Ardhi itasimamia ardhi hiyo kwa niaba yao.

(4)Ardhi ya umma haitatolewa au kutumiwa isipokuwa kwa kuzingatia Sheria ya Bunge inayofafanua hali na masharti ya kutolewa au matumizi hayo.

Isome ndani ya Sura ya Tano →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho