Katiba ya Kenya, 2010

Sura ya Tano · Ardhi na Mazingira

Kifungu cha 63

Kif.63

Ardhi ya jamii

(1)Ardhi ya jamii itamilikiwa na jamii zinazotambuliwa kwa misingi ya kikabila, kitamaduni au mahitaji sawa ya kijamii.

(2)Ardhi ya jamii inajumuisha—

(a)ardhi iliyosajiliwa kisheria kwa jina la wawakilishi wa kikundi chini masharti ya sheria yoyote;

(b)ardhi iliyokabidhiwa jamii fulani kisheria na kupitia kwa mchakato wowote wa kisheria;

(c)ardhi nyingine yoyote itakayotangazwa na Sheria ya Bunge kuwa ardhi ya jamii ; na

(d)ardhi ambayo—

(i)inamilikiwa kwa uhalali, inasimamiwa au kutumiwa na jamii maalum kama misitu ya jamii, maeneo ya malisho ya mifugo au mahali patakatifu pa ibada;

(ii)ni ya kiasili na ardhi ambayo kiasili inamilikiwa na jamii ya wawindaji; au

(iii)inamilikiwa kisheria kama ardhi ya amana na serikali za kaunti, lakini isiyojumuisha ardhi yoyote ya umma inayomilikiwa na serikali ya kaunti kwa niaba ya wakazi wa kaunti hiyo chini ya Kifungu cha 62 (2).

(3)Ardhi yoyote ya jamii ambayo haijasajiliwa itamilikiwa na serikali za kaunit kwa niaba ya jamii hizo.

(4)Ardhi ya jamii haitatolewa au kutumiwa vinginevyo isipokuwa kulingana na sheria inayofafanua hali na viwango vya haki za kila mwanajamii kibinafsi au wanajamii wote kwa pamoja.

(5)Bunge litatunga sheria kuwezesha utekelezaji wa Kifungu hiki.

Isome ndani ya Sura ya Tano →

Maandishi: Tafsiri ya Kiswahili ya Katiba ya Kenya, 2010, iliyochapishwa na Uraia kwa kutumia chapisho la Halmashauri ya Kitaifa ya Kuripoti Maswala ya Sheria (27 Agosti 2010). Ikiwa kuna utata wowote kuhusu tafsiri, nakala ya Kiingereza ndiyo rasmi.

Huu ni msaada wa kusoma, si ushauri wa kisheria. Kwa swali la kisheria, ongea na wakili. Umeona kosa? Ripoti marekebisho